Friday, March 2, 2018

Nyongo ataka madini ya nickel yaongezwe thamani nchini


Na Veronica Simba, Ngara

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Serikali itaboresha mazingira ya uwekezaji wa Madini ya Nickel yanayopatikana Ngara mkoani Kagera lakini pia itahakikisha wawekezaji wanayaongezea thamani Madini hayo hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi ili kuleta tija zaidi.

Aliyasema hayo jana, Machi Mosi alipotembelea Mradi wa Uwekezaji wa Madini ya Nickel wa Kabanga, uliopo wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, akiwa katika ziara ya kazi.

“Sisi kama Serikali tutahakikisha tunawaletea wawekezaji miundombinu ya Barabara, Reli na Umeme ili kuwajengea mazingira rafiki ya uzalishaji lakini kwa upande wao tunataka kuona uwekezaji makini; wachimbe na kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini. Badala ya kutoa Nickel kama malighafi, watoe bidhaa zinazotokana na Nickel.”

Alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha Madini hayo muhimu, ambayo kwa sasa Soko lake Duniani limeanza kupanda, yanalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili.

Akifafanua, Naibu Waziri alisema kuwa, Nickel ikiongezewa thamani hapa nchini, miundombinu ya Reli, Umeme na Barabara ikaboreshwa; kutakuwa na uhakika wa kuuza Madini hayo kwa bei nzuri na kuleta ushindani kwenye Soko la Dunia.

“Tunataka wawekezaji wachimbe ili tupate kodi, tupate mrabaha lakini pia wananchi wa maeneo haya waweze kupata ajira.”

Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki katika ziara hiyo, ambaye alitaka kujua Serikali ina mtazamo gani kuhusu umakini wa mwekezaji aliyepo sasa, Naibu Waziri alisema kuwa Serikali inamchukulia mwekezaji huyo kama mwekezaji makini kutokana na namna alivyojipambanua katika shughuli hiyo.

“Mtu ambaye amewekeza kiasi cha Dola Milioni 275 hadi kufikia sasa, sioni kwamba anatania katika uwekezaji. Namwona ni mwekezaji aliyedhamiria na aliye makini.”

Hata hivyo, Nyongo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kukaribisha wawekezaji wengine makini katika sekta hiyo ili kwa pamoja wasaidie kuinua Pato la Taifa kupitia uwekezaji wao.

Awali, akiwasilisha Taarifa ya utendaji kazi wa Mradi wa Kabanga Nickel, Meneja Mkazi wa Mradi huo, Andrew Msola alimweleza Naibu Waziri kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni ukosefu wa miundombinu muhimu ya Barabara, Reli pamoja na Umeme; ambapo Naibu Waziri aliahidi Serikali kushughulikia suala hilo kwa haraka.

Ilielezwa kuwa Mradi wa Kabanga Nickel ulianza uzalishaji wa Madini ya Nickel zaidi ya miaka 40 iliyopita, lakini tangu mwaka 2009 ilisimamisha uzalishaji kutokana na kuporomoka kwa bei ya Madini hayo katika Soko la Dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Waziri aliwaeleza kuwa, kwa sasa Soko la Madini hayo limeanza kuimarika kutokana na kukua kwa teknolojia ambayo imesababisha kuongezeka kwa matumizi ya Madini ya Nickel ikiwemo kutumika katika Magari ya Umeme badala ya yale yanayotumia mafuta.

“Mathalani Miji mikubwa ya Ulaya hivi sasa, wanataka waachane na Magari yanayotumia mafuta na kujikita kwenye yale yanayotumia Betri zinazochajiwa kwa umeme. Aidha, Dunia nzima sasa inazungumzia suala la utunzaji wa mazingira, hivyo kila mmoja anataka kuachana au kupunguza matumizi ya mafuta ili kutunza mazingira.”

Baada ya Kagera, Naibu Waziri ameelekea Mkoa wa Kigoma ambako anatarajia kuhitimisha ziara yake. Awali, katika ziara hiyo, alitembelea Mikoa ya Mwanza na Geita.


Meneja Mkazi wa Mradi wa Kabanga Nickel, Andrew Msola akiwasilisha Taarifa ya Utendaji kazi wa Mradi huo kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Ujumbe aliofuatana nao, alipotembelea na kukagua Mradi huo akiwa katika ziara ya kazi, Machi Mosi mwaka huu.


Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mlengele, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Ngara Alex Gashaza na Afisa Madini Mkazi wa Kagera Daniel Mapunda, wakiwa katika kikao na Wawekezaji wa Mradi wa Kabanga Nickel wakati wa ziara ya Naibu Waziri, Machi Mosi mwaka huu.


Sehemu ya shehena ya Madini ya Nickel kama ilivyokutwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), katika Mradi wa Kabanga Nickel, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera, Machi Mosi mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kukagua Mradi wa Kabanga Nickel uliopo Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Machi Mosi mwaka huu akiwa katika ziara ya kazi.

No comments:

Post a Comment