Na
Veronica Simba, Kakonko
Wananchi wa Wilaya ya
Kakonko, Mkoani Kigoma, wameiomba Serikali isaidie kuwapatia wataalam wa
miamba, ili wafanye utafiti utakaobainisha kiasi cha madini yaliyogundulika
kuwepo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.
Akiwasilisha Taarifa
ya Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, aliyefika ofisini
kwake na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama, akiwa katika ziara ya kazi
jana Machi Mosi, Mkuu wa Wilaya Kanali Hosea Ndagala alisema kuwa Madini ya
Dhahabu yamegundulika katika maeneo mbalimbali, hususan Nyamtukuza, Kasuga na
Muhange lakini haijaweza kufahamika ni kiasi gani kilichopo.
“Tunakuomba utusaidie
upatikanaji wa wataalam ili kujua takwimu sahihi za kiasi cha Madini hayo
kilichopo kwenye maeneo yaliyogundulika.”
Aidha, Kanali Ndagala
alitaja changamoto nyingine katika Wilaya hiyo kuwa ni uwepo wa hazina kubwa ya
Madini ya Chokaa katika Hifadhi ya Pori la Akiba la Moyowosi, lakini imekuwa
vigumu kufanya shughuli za uchimbaji kutokana na Sheria za Hifadhi.
“Kwa namna ya pekee
tunakuomba utusaidie eneo hilo litolewe ridhaa ya kufanyika shughuli za
uwekezaji na uchimbaji ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa viwanda, kutoa
nafasi za ajira na kuinua vipato vya wananchi katika Wilaya yetu,” alisema.
Akijibu maombi
husika, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake, hivi
sasa imejipanga kufanya tafiti mbalimbali za Madini nchini kote kwa kuwatumia
wataalam wa jiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
Akifafanua zaidi,
alisema kuwa lengo la Serikali ni kuweza kuainisha maeneo yote yenye madini,
kutoa ushauri na hata kukaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo husika kwa
maana ya kuwapa taarifa sahihi za kijiolojia.
“Hivyo basi,
tutawaelekeza wataalam wetu wafike hapa Kakonko pia na kufanya utafiti,”
alisema Nyongo.
Kuhusu upatikanaji wa
Madini ya Chokaa katika eneo la Hifadhi, Naibu Waziri aliahidi kulifanyia kazi
suala hilo ili kuona kama kuna uwezekano wa kutolewa ridhaa ya kuchimbwa Madini
hayo kwani alisema yanahitajika sana kwa sasa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri alieleza kuwa, kutokana na Mheshimiwa Rais John Magufuli
kuifanya Wizara ya Madini kujitegemea na kusimama peke yake, kutoka iliyokuwa
Wizara ya Nishati na Madini; jukumu la Wizara hiyo mpya sasa ni kuhakikisha
Madini yanalinufaisha Taifa ipasavyo.
“Macho yetu sasa ni
kwenye Madini tu. Tunataka kuhakikisha kwamba kila Mkoa hapa nchini unachangia
katika Pato la Taifa kupitia shughuli za Madini kwani nchi yetu imejaaliwa kuwa
na Madini mbalimbali katika Mikoa karibu yote.”
Akielezea ziara yake
katika Mkoa huo wa Kigoma, Nyongo alisema itahusisha pia kutembelea na kujionea
shughuli za uchimbaji wa Madini Chumvi zinazofanyika Uvinza.
Akifafanua, alisema
kuwa nchi imekuwa ikiagiza kiasi kikubwa cha Chumvi kutoka nje wakati Madini
hayo yanapatikana hapa nchini, hivyo Serikali imedhamiria kuhakikisha
inawezesha uzalishaji wa kutosha wa Chumvi bora hapa nchini itakayotosheleza
mahitaji ya Soko la ndani.
Naibu Waziri Nyongo
anaendelea na ziara yake ambayo itahitimishwa mkoani Kigoma. Mikoa mingine
aliyotembelea katika ziara hiyo ni Mwanza, Geita na Kagera.
No comments:
Post a Comment