Monday, March 5, 2018

Nyongo aagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi mgogoro wa ruzuku


Na Veronica Simba, Kasulu

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa maagizo kwa Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kuchunguza madai ya wanachama wa Kikundi cha Wachimbaji Chokaa cha Makere wilayani humo; kwamba mmoja wao amewageuka na kutumia peke yake, fedha za ruzuku zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kikundi hicho.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo jana, Machi 2, baada ya kupokea Taarifa ya Kikundi husika iliyowasilishwa na Francis Buhaga kwa niaba ya wanachama wenzake.

Alisema kuwa, malalamiko hayo yanapaswa yashughulikiwe kisheria ili haki itendeke, pasipo upande wowote kuonewa.

“Huu ni uhuni umefanyika. Afisa Takukuru aifuatilie kesi hii bila kumwogopa mtu. Haki itendeke na sheria ichukue mkondo wake.”

Akieleza zaidi, Nyongo alisema kuwa nia ya Serikali kuwapatia wachimbaji ruzuku ilikuwa ni njema lakini ni kwa matatizo kama hayo, Mheshimiwa Rais John Magufuli aliamua zoezi hilo lisitishwe hadi pale hali itakapodhihirika kutulia.

“Wengine wanapewa fedha, wanaenda kuzitumia kwa matumizi yao binafsi kama ilivyofanyika hapa kwenye Kikundi chenu. Haya mambo yapo na baadhi ya Ofisi zetu za Madini zilikuwa zinashiriki. Mathalani, haiingii akilini, kwamba Kikundi kikose sifa ya kupewa ruzuku halafu mtu mmoja awe na sifa hizo na apewe hela, Sisi kama Serikali, hilo hatuwezi kukubali,” alisisitiza.

Aidha, akifafanua masuala yanayopaswa kufanyiwa uchunguzi na Takukuru katika mgogoro husika, Naibu Waziri alisema kuwa ni pamoja na kuchunguza ni nani alihongwa pamoja na kiasi halisi cha pesa iliyotolewa, “Maana nimesikia haikufika Milioni 50 kwenye Kikundi, kuna nyingine ilikatwa. Ichunguzwe aliyepewa ni nani.”

Vilevile, aliitaka Takukuru kuchunguza ilikuwaje mwana-kikundi huyo akajenga Ghala lake binafsi kwenye Kiwanja cha Kikundi.

“Tumieni muhtasari wa vikao vya Kikundi vilivyofanyika awali kwa ajili ya kuomba hiyo ruzuku. Kama anastahili kwenda Mahakamani, apelekwe Mahakamani, kama ana haki yake, basi Mahakama itaitambua. Maana Mahakama ipo kwa ajili ya kutafsiri sheria. Kwahiyo, asionewe mtu.”

Awali, katika uwasilishaji wa Risala yao kwa Naibu Waziri, wanachama wa kikundi hicho walieleza kuwa, mwaka 2015 walifanikiwa kupata ruzuku ya Serikali kiasi cha shilingi Milioni 50, ambazo zilitumika kujenga Ghala la kuhifadhia Chokaa ya Kikundi na kununulia vifaa mbalimbali vya kuendeshea shughuli zao.

Aidha, walidai kwamba pamoja na ruzuku hiyo, wana-Kikundi walichangia gharama na vifaa mbalimbali zenye thamani ya jumla ya shilingi 4,955,000.

“Baada ya shughuli za ujenzi wa Ghala kukamilika na kufunga mitambo, tunashangaa na kusikitika kwa kunyang’anywa Mradi huo na kumilikiwa na mchimbaji mmoja akidai kuwa ruzuku hiyo ni mali yake peke yake.”

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Madini Kigoma, Mkaguzi wa Migodi kutoka Ofisi hiyo, Laurent Bujashi alimweleza Naibu Waziri kuwa ni kweli ruzuku hiyo ilitolewa kwa mwanachama mmoja kwani ndiye aliyekuwa akikidhi vigezo, lakini kwa ahadi kuwa atashirikiana na wana-kikundi wenzake.

Kwa upande wake, mwanachama huyo anayetuhumiwa kuwageuka wenzake, alimweleza Naibu Waziri kuwa, alipewa ruzuku hiyo kutokana na kukidhi vigezo vilivyotakiwa, ambavyo wanakikundi wenzake hawakuwa navyo; na kwamba alidhamiria kushirikiana na wenzake hao, lakini walimgomea wakidai kuwa hawawezi kujumuika naye kwani watakuwa wanamsaidia kukuza jina lake, hivyo akaamua kuendesha Mradi husika yeye mwenyewe.

Wachimbaji hao pia walimwomba Naibu Waziri awasaidie kupata ruhusa ya Serikali ili waendeleze shughuli za uchimbaji katika eneo la Msitu wa Hifadhi ulioko Makere, ambapo Naibu Waziri aliahidi kuwa Wizara yake itakutana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuzungumzia namna bora ya kupata suluhisho kwa changamoto hiyo kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kushoto), akikagua Ghala la kuhifadhia Madini ya Chokaa, linalodaiwa kujengwa na mmoja wa wanachama wa Kikundi cha Wachoma Chokaa Makere (katikati) katika Kiwanja cha Kikundi kwa matumizi yake pekee. Kulia ni Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Method Venance.


Wanachama wa Kikundi cha Wachoma Chokaa Makere (kulia), wakimpokea Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kushoto), alipowasili katika eneo hilo lililopo Kasulu kuzungumza nao na kujionea shughuli wanazofanya, akiwa katika ziara ya kazi, Machi 2 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia), akipokea Risala ya Kikundi cha Wachoma Chokaa Makere, kutoka kwa mmoja wa wanakikundi, Francis Buhaga (kushoto). Naibu Waziri aliwatembelea Wachimbaji hao wa Chokaa kujionea shughuli zao na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Machi 2 mwaka huu.


Wanachama wa Kikundi cha Wachoma Chokaa Makere, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), alipowatembelea kujionea shughuli zao na kuzungumza nao akiwa katika ziara ya kazi wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Machi 2 mwaka huu.


Mkaguzi Migodi kutoka Ofisi ya Madini Kigoma, Laurent Bujashi akizungumza, wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) na wachimbaji wa Madini ya Chokaa wa Makere wilayani Kasulu (hawapo pichani), Machi 2 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment