Na
Veronica Simba, Kigoma
“Ni fursa kubwa sana
kwa wananchi wa Kigoma. Wasidhani kwamba fursa iliyopo hapa ni ya uvuvi na
mawese peke yake; wanaweza kuwa matajiri wakubwa kupitia Madini ya Chokaa na
Chumvi.”
Akifafanua zaidi,
Nyongo alisema kuwa, katika siku mbili za ziara yake mkoani Kigoma, ameshuhudia
maeneo mengi yenye Chokaa ya kutosha na kwamba uzalishaji wake ni rahisi sana
kwani kinachohitajika ni kuyachoma mawe husika na kusaga; basi.
Akizungumzia upande
wa Chumvi, alisema kuwa, Mgodi wa kuzalisha Chumvi wa Nyanza, uliopo Uvinza unafanya
kazi nzuri katika uzalishaji lakini kwa bahati mbaya asilimia 70 ya bidhaa
wanayozalisha, huiuza nje ya nchi hususan katika nchi jirani za Kongo na
Burundi.
Alisema kuwa, pamoja
na kwamba wawekezaji hao wanalazimika kuuza asilimia kubwa ya chumvi yao nje ya
nchi kutokana na sababu za kijiografia na miundombinu ya usafirishaji; Serikali
inaona suala hilo siyo sawa, hivyo inaweka mikakati kuhakikisha wazalishaji hao
na wengine wote wanatosheleza Soko la Ndani ya nchi kwanza; ambalo ni kubwa,
kabla ya kuuza nje.
“Mahitaji ya Chumvi
kwa Tanzania ni takribani tani 250,000 kwa Mwaka na takwimu zilizopo zinaonesha
tunaagiza kiasi kikubwa cha Chumvi kutoka nje ya nchi, hususan Kenya, wakati
hii ya kwetu tunayozalisha nchini, tunaiuza nje. Hii siyo sawa. Ni lazima sasa
tuweke mikakati itakayowezesha wawekezaji wetu kutosheleza Soko la Ndani
kwanza,” alisisitiza.
Kuhusu mikakati
ambayo Serikali inaifanya katika kuboresha sekta hiyo ndogo ya chumvi; Naibu
Waziri alisema kuwa, ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogowadogo, waweze
kuzalisha chumvi nyingi itakayotosheleza Soko la Ndani na la Nje.
“Mathalani,
tumedhamiria kufungua Vituo vya Mfano (Centre of Excellence) sehemu mbalimbali
nchini. Tumekwishaanza na Lindi, tutafanya hivyo kwa Mikoa mingine ikiwemo huu
wa Kigoma ili wachimbaji wajifunze namna ya uzalishaji bora wa chumvi ikiwemo
kuiongezea madini joto, ambao ni mkakati wa kidunia pamoja na kuifungasha
katika hali ya ubora iweze kukidhi viwango vya Soko la Ndani na hata vya
ushindani katika Soko la Nje.”
Aidha, Naibu Waziri
alisema kuwa, ili kuwawezesha zaidi wawekezaji katika sekta husika; Serikali
kupitia Wizara ya Madini pamoja na Idara nyingine zinazohusika, watakaa pamoja
wajadili namna wanavyoweza kupunguza wingi wa kodi zinazotajwa kufikia 14 na
kulalamikiwa na wawekezaji, ili waweze kufanya biashara hiyo kwa tija zaidi.
Alisema kuwa, ni
suala linaloleta ‘ukakasi’ kuona wingi wa kodi inayotozwa kwa wazalishaji wa
chumvi wa ndani ya nchi na wakati huohuo nchi inaagiza chumvi kutoka nje pasipo
kodi yoyote, hivyo akasisitiza kuwa Serikali imeona kuna umuhimu mkubwa kwa
wadau kukutana, kujadili na kuweka mikakati itakayoleta suluhisho lenye tija.
Wizara ya Madini
imekuwa ikieleza dhamira yake ya kuhakikisha uchangiaji wa sekta hiyo katika
Pato la Taifa unakua zaidi ya ilivyo sasa, kupitia usimamizi mzuri
utakaowezesha ongezeko la wawekezaji wenye kulipa kodi na tozo zote stahiki za
Serikali.
Sehemu ya Shamba la Chumvi la Mgodi wa Nyanza Salt uliopo Uvinza. Picha hii ilipigwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) Mgodini hapo, Machi 3 Mwaka huu. |
No comments:
Post a Comment