Na
Veronica Simba, Kigoma
Wachimbaji wa Madini
wadogo wa Mkoa wa Kigoma, wamemweleza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao na kumwomba awasaidie
kuzitatua.
Walimweleza
changamoto hizo katika kikao maalum, Machi 3 mwaka huu, wakati Naibu Waziri
alipowatembelea akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo.
Miongoni mwa
changamoto kubwa waliyoitaja ni kuhusu vibali vya kusafirisha madini ghafi nje
ya nchi; ambapo Naibu Waziri aliwataka kuwa wavumilivu kwani Serikali
inakamilisha mchakato wa kuandaa Mwongozo maalum utakaopambanua kila aina ya
madini yaliyo nchini na yanapaswa kusafirishwa yakiwa katika hali gani.
“Unajua, Madini
yanatofautiana, na uchakataji wake unatofautiana. Hivyo tumeona tuandae
Mwongozo utakaoondoa mkanganyiko huo na kuwarahisishia kujua Madini gani
yanapaswa kuongezewa thamani kwa kiwango kipi ili uruhusiwe kuyasafirisha nje
ya nchi.”
Alisema kuwa,
Mwongozo huo utatolewa hivi karibuni na hivyo Serikali itaanza tena kutoa
vibali vya usafirishaji Madini nje ya nchi.
Vilevile, wachimbaji
hao walitaja changamoto nyingine kuwa ni upatikanaji wa Ruzuku ambapo pamoja na
kulalamikia Serikali kusimamisha zoezi hilo, lakini pia walidai kuwa wakati
ikitolewa, wahusika hawakutenda haki.
“Wasiokuwa na vigezo
ndiyo walikuwa wakipatiwa Ruzuku ilhali wenye vigezo wakinyimwa,” walilalamika.
Akizungumzia suala
hilo, Naibu Waziri aliwaeleza kuwa Serikali iliamua kusimamisha kwa muda zoezi
la utoaji Ruzuku kutokana na kugundua udhaifu katika zoezi husika ikiwemo
baadhi ya wanufaika kutumia Ruzuku waliyopewa kwa mambo yao binafsi tofauti na
masharti yake. Hata hivyo, alisema kuwa Ruzuku itaanza kutolewa tena baada ya
Serikali kujiridhisha kuwa itatumika vema.
Kuhusu suala la wenye
vigezo kunyimwa Ruzuku na wasio na vigezo kupatiwa; Naibu Waziri alisema
Serikali itafuatilia na kuchunguza kwa ukaribu ili kuwabaini watumishi wa umma
na wengine wanaoshirikiana nao katika kupindisha utaratibu uliowekwa kwa sababu
wanaozijua wao.
“Tukiwabaini
tutawachukulia hatua kali za kisheria. Nanyi tunawaomba mtuletee aina yoyote ya
ushahidi unaoweza kutusaidia kuthibitisha madai yenu ili kwa pamoja tukomeshe
tatizo hilo.”
Aliongeza kuwa,
katika kushughulikia tatizo hilo, tayari Serikali ilishatoa tamko kuwataka wale
waliotumia Ruzuku kwa matumizi binafsi tofauti na masharti yake, wazirudishe
pesa hizo mara moja na kwamba muda waliopewa kurudisha umekwisha, hivyo
wataanza kushughulikiwa.
Wachimbaji hao pia walilalamikia
kutopewa ushirikiano na watumishi wa Ofisi ya Madini Kigoma ambapo Naibu Waziri
aliahidi kufuatilia na kushughulikia suala hilo.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji madini wadogo wa Mkoa wa Kigoma, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani humo, Machi 3 Mwaka huu. |
No comments:
Post a Comment