Na Mohamed Saif,
Serikali imesema inapitia upya
Leseni zote za Utafiti wa Madini kwenye Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita ili
kubaini ambazo hazijaendelezwa ili zifutwe na maeneo hayo kutengwa kwa ajili ya
kuwapatia wachimbaji wadogo.
Naibu Waziri wa Madini,
Doto Biteko amebainisha hayo hivi karibuni wakati wa mkutano na wachimbaji
wadogo wa Kijiji cha Bululu, Kata ya Nyamtukuza wilayani humo.
Akizungumza kwa niaba ya
wachimbaji hao, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, Hussein Amar alisema wananchi
wa wilaya hiyo wanateseka kwa kukosa maeneo ya kuchimba madini na kwamba
wamekuwa wakikimbizwa kwenye maeneo waliyokuwa wakifanya uchimbaji kwa madai
kuwa maeneo hayo yanamwenyewe.
Akijibu maombi hayo,
Biteko alisema Rais John Magufuli anataka kuona Watanzania wanyonge wananufaika
na rasilimali zao ikiwemo rasilimali madini.
“Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ni Serikali inayowaangalia
wanyonge. Haitaki Watanzania wanyonge waendelee kuteseka na kunyanyaswa. Muda
umefika Watanzania nao wanufaike,” alisema Biteko.
Alifafanua kuwa Sheria
ya Madini iliyokuwa ikitumika hapo awali kabla ya Marekebisho ya Mwaka 2017,
haikumpa haki Mtanzania lakini hivi sasa inatamka bayana kwamba rasilimali zote
ikiwemo madini ni mali ya Watanzania
Mara baada ya kufafanua
hayo, Biteko alibainisha kuwa kwenye Mkoa wa Geita kila wilaya yapo maeneo
kadhaa yametengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo isipokuwa kwa Wilaya ya
Nyang’wale kwakuwa maeneo mengi wilayani humo tayari yana leseni.
Hata hivyo alifafanua
kuwa leseni za maeneo wanayohitaji wachimbaji hao zitamaliza muda wake siku
chache zijazo “Maeneo mnayohitaji yana leseni; zipo za utafiti na zingine za
uchimbaji lakini habari njema ni kwamba zote zinamaliza muda wake,” alisema.
Aliwataka wachimbaji hao
kufanya subira kwani maeneo wanayohitaji leseni zilizopo zinamaliza muda wake
Machi 30 Mwaka huu na ndipo mpango wa kugawa maeneo hayo utakapofanyika.
Akielezea utaratibu
utakaotumika kwenye ugawaji wa maeneo hayo, Biteko aliwataka wachimbaji
hao waingie kwenye mfumo rasmi wa kuunda vikundi na wawasilishe
orodha ya vikundi hivyo kwa Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Madini ili kuanza mara
moja mpango na utaratibu wa ugawaji wa maeneo husika.
“Ugawaji wa maeneo
utazingatia vikundi na sio mtu mmoja mmoja ili iwe rahisi pia kupatiwa msaada
na Serikali. Kama hamna vikundi undeni sasa na muwasilishe orodha ili taratibu
za ugawaji zifanyike,” alisema.
Vilevile aliwakumbusha
wajibu wao wa kufuata maelekezo ya Serikali na kulipa kodi sambamba na kuacha
tabia ya kutorosha madini. “Ni ushamba kutorosha madini, mtu mjanja ni yule
anaelipa kodi ili Serikali ipate fedha ya kuwahudumia wananchi mkiwemo na
nyinyi wachimbaji wadogo,” alisema.
Aidha, Naibu Waziri
Biteko aliweka bayana kwamba maeneo ambayo hayaendelezwi na hakuna taarifa
yoyote iliyowasilishwa kwenye Ofisi za Madini, leseni kwenye maeneo hayo
zitafutwa mara moja na maeneo hayo kupatiwa wenye nia ya dhati ya kuyaendeleza.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa Bululu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani). |
Naibu Waziri wa madini, Doto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa Bululu (hawapo pichani). |
Naibu Waziri wa madini, Doto Biteko
akizungumza na wachimbaji wadogo wa Bululu (hawapo pichani).
|
No comments:
Post a Comment