Na Mohamed Saif
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipongeza Kampuni ya Mzawa ya Nyamigogo Grand
Vezir Holdings Ltd inayojishughulisha na uchenjuaji dhahabu kwa kuthubutu
kuanzisha mradi huo na aliahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili
kuona manufaa zaidi yakipatikana.
Alitoa
pongezi hizo Machi 6, 2018 alipofanya ziara kwenye mgodi huo uliopo Wilayani
Nyang’hwale Mkoani Geita ili kujionea shughuli ziazoendelea sambamba na
kuzungumza na watendaji wake.
Biteko
aliitaka kampuni hiyo kuendelea kufuata maelekezo ya Serikali ikiwemo kufuata
sheria, kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali sanjari na kutunza takwimu
za uendeshaji wa shughuli zao kwa mujibu wa matakwa ya sheria.
Mara baada
ya kupokea taarifa ya mgodi huo, Biteko aliahidi kushughulikia changamoto
mbalimbali zinazoukabili mgodi huo ikiwemo suala la maeneo ya uchimbaji na
upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme.
“Suala la
umeme nitalifikisha; tunahitaji kuona maendeleo. Tunahakikisha tunaandaa mazingira
mazuri kwa wawekezaji wote wa ndani na nje,” alisema Biteko.
Kuhusu
suala la maeneo, Biteko alisema wenye maeneo ambayo hawayaendelezi watafutiwa
leseni na maeneo hayo kugawiwa upya kwa wenye nia ya dhati ya kufanya maendeleo
ikiwemo kampuni hiyo.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Kampuni, Hussein Amar alimueleza Naibu Waziri Biteko
mafanikio yaliyofikiwa tangu mradi huo uanze kufanya kazi Mwaka 2013 ikiwemo
ajira kwa wananchi wa maeneo ya karibu na Watanzania kwa ujumla ambapo alisema
mradi umeajiri wafanyakazi wapatao 60.
Amar
aliongeza kuwa mradi huo unaunga mkono jitihada za maendeleo ikiwemo kuchangia
ujenzi wa vyumba vya viwili vya madarasa katika Sekondari ya Izunya, ujenzi wa
Zahanati, ujenzi wa Ofisi ya Mtendaji Kitongoji cha Ibalangulu na uanzishaji wa
mradi wa ufugaji nyuki kwa wananchi wanaozunguka mradi.
Aidha,
Amar alizungumzia changamoto mbalimbali zinazoukabili mradi huo ikiwemo ukosefu
wa maeneo ya uchimbaji hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo unafunga mitambo ya
kuchenjulia dhahabu yenye uwezo wa kusaga mawe kiasi cha Tani 500 kwa Saa 24 na
kwamba inahitaji maeneo ili kufanya uchimbaji utakaokidhi mahitaji ya
uendeshaji wa mitambo hiyo.
Aliomba kusogezewa
huduma ya nishati ya umeme kwakuwa gharama kubwa inatumika kununulia mafuta kwa
ajili ya kuzalisha umeme hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi zinazofanyika
mgodini hapo zinahitaji nishati ya umeme.
Alisema
endapo huduma hiyo ya nishati itapatikana, mgodi utazalisha ajira zaidi kwani
uendeshaji wake utakuwa wa muda mrefu kwa kuwa na awamu nyingi (work shifts
addition) na kwamba mgodi huo kwa sasa umeajiri wafanyakazi 60.
“Tunazalisha
umeme wetu kwa kutumia mafuta; hii inasababisha gharama za uendeshaji kuwa
kubwa. Tunaomba Serikali itusogezee huduma ya nishati ili kupunguza gharama za
uendeshaji,” alisema Amar.
Naibu
Waziri Biteko amekamilisha ziara yake Mkoani Geita ambapo alitembelea maeneo
mbalimbali ya uchimbaji ili kujionea shughuli zinazofanyika na kuzungumza na
wachimbaji kwa utatuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment