Ø Nyongo awataka wachague moja;
kuwalipa wananchi waondoke au waruhusiwe kuendeleza maeneo yao
Ø Mchakato kuwalipa waathirika wa
milipuko uanze mara moja
Na
Veronica Simba – Geita
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM),
kuanza mara moja mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Nyamalembo
mjini Geita, ambao nyumba zao zimeathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi
huo.
Aidha, Naibu Waziri
ameutaka Mgodi huo kuchagua moja kati ya kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha
Nyakabale ambacho kipo ndani ya eneo la Leseni yao, ili waondoke au kutoa tamko
la kuwaruhusu kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika eneo hilo.
Nyongo ametoa maagizo
hayo Februari 23 na 24 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Geita,
ambapo alikutana na wananchi wa maeneo husika kujionea hali halisi, kuzungumza
nao na kisha kukutana na uongozi wa GGM.
“Naagiza, kuanzia
Jumatatu Februari 26, ninyi GGM kwa kushirikiana na Timu iliyofanya uthamini wa
nyumba zilizoathiriwa pamoja na ile Timu ya Serikali, mkae pamoja kuandaa
mchakato wa kuwalipa wananchi hawa. Suala hilo nitalisimamia ili kuhakikisha
wote ambao nyumba zao zimeathiriwa wanapatiwa fidia.”
Nyongo alisema
anatambua kuwa GGM wanatumia kigezo cha sheria na kanuni inayowaruhusu kutolipa
fidia ya ardhi katika maeneo ambayo bado hawajaanza kuyafanyia kazi, lakini
hata hivyo aliwataka kutumia kigezo cha ubinadamu na uhusiano mwema kuwalipa wananchi
hao.
Alitahadharisha
kwamba, yawezekana kukawa na udhaifu au upungufu katika sheria na kanuni
mbalimbali zinazoongoza sekta husika, na kwamba wako baadhi ya watu wanaotumia
mwanya huo kuwakandamiza wengine, hususan wananchi.
“Sasa kama kuna
sheria na kanuni zinazombana mwananchi, tuko tayari kuzirekebisha. Hata hivyo,
nawaasa, msitumie udhaifu wa sheria kumkandamiza mwananchi wa kawaida.”
Naibu Waziri Nyongo
alisema Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi makini wa Rais John
Magufuli, haiwezi kukubali kuona mwekezaji yeyote anakuwa kero kwa wananchi.
“Hatuko tayari
kumwona mwananchi anaonewa na mwekezaji. Tunataka watu waishi kwa amani,
wafurahie uwekezaji ambao tumeukaribisha. Hatutasita kukuchukulia hatua wewe
ambaye unatumia udhaifu wa sheria kumwonea mwananchi.”
Akizungumzia umuhimu wa
kujenga uhusiano mzuri na amani ya kudumu baina ya wawekezaji na jamii
inayowazunguka, Nyongo alisema kuwa suala hilo linawezekana endapo kutakuwa na
utaratibu wa mazungumzo na makubaliano ya masuala mbalimbali kati ya pande zote
husika.
Hata hivyo, Naibu
Waziri alibainisha kuwa lengo la Serikali siyo kuwafukuza wawekezaji bali ni
kuhakikisha wanafanya kazi yao ya uwekezaji pasipo kuwakandamiza wananchi.
Alisema kuwa, ni
lazima pande zote mbili zihakikishe zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa,
lakini wasisahau kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Akizungumzia tabia ya
baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya leseni za wawekezaji wakubwa,
Nyongo alisema kuwa siyo sahihi na kuwataka kuacha mara moja kwani ni kinyume
cha sheria.
“Wako wanaopotosha kauli
na agizo la Mheshimiwa Rais wetu, aliposema kuwa wachimbaji wadogo walio katika
maeneo yao wasibugudhiwe bali waachwe waendelee na kazi yao ya uchimbaji katika
maeneo hayo. Naomba ieleweke kuwa, Mheshimiwa Rais hakusema mwende mkavamie
leseni za wawekezaji bali mbaki katika maeneo yenu, na yeyote asiwaondoe.”
Akifafanua zaidi,
alisema kuwa, Serikali imeanzisha Kamisheni maalum itakayoshughulikia sekta ya
madini, na kwamba inatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni. Aliwataka
wachimbaji wadogo wasio na leseni wahakikishe wanafuata taratibu husika mara tu
Kamisheni hiyo itakapoanza kufanya kazi ili wapate leseni na kurasimishwa
katika kazi hiyo.
Alisema kuwa,
Serikali inataka kuona wachimbaji wote wa madini wanafanya kazi zao kwa amani
ili walipe kodi na tozo zote stahiki ili kuwezesha kuongeza mchango wa sekta
hiyo katika Pato la Taifa.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri aliuagiza Mgodi wa GGM kuzingatia umuhimu wa kuwawezesha
wananchi wanaowazunguka na Taifa kwa ujumla kwa kutumia na kutoa kipaumbele kwa
bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi na maeneo ya jirani kwani suala
hilo lipo kisheria.
Awali, akizungumza katika
ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi,
Mhandisi Yahya Samamba alisema mgogoro husika umekuwa wa muda mrefu hivyo ni
wakati muafaka hatua stahiki zikakamilishwa ili kurejesha amani katika eneo
hilo.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi pamoja na kupongeza maagizo yote yaliyotolewa
na Naibu Waziri, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uwazi, upendo na utashi kwa
pande zote mbili ili kuhakikisha kunakuwa na suluhisho la kudumu la migogoro
husika.
Mbunge wa Geita
Mjini, Costantine Kanyasu, aliishukuru Serikali kwa dhamira ya dhati
iliyoonesha ya kushughulikia migogoro hiyo ambayo alisema imekuwa
ikiwasononesha wananchi wa Geita kwa muda mrefu.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyakabale –
Geita, wakati wa ziara yake ya kazi, Februari 24 mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment