Na
Veronica Simba, Arusha
Serikali imesema iko
tayari kurekebisha mapungufu yatakayobainika katika Sheria au Kanuni za Madini
ili kuhakikisha wadau wote wa sekta hiyo wananufaika ipasavyo hivyo kukuza Pato
la Taifa.
Hayo yalisemwa
Februari 14 jijini Arusha na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto
Biteko wakati wa Mkutano wao na wadau wa sekta ya madini wakiwemo Chama cha
Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini
Tanzania (FEMATA).
Akizungumzia suala
hilo, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini
haitasita kufanya marekebisho katika sheria au kanuni za madini zitakazobainika
kuwa kikwazo katika biashara ya madini nchini.
Akiunga mkono maneno
hayo, Naibu Waziri Biteko alisema “Sheria au Kanuni siyo Msahafu ambao hauwezi
kubadilishwa hivyo pale tutakapojiridhisha kuna mapungufu, tutarekebisha kusudi
mambo yaende vizuri.”
Biteko na Nyongo
walisema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya madini inalinufaisha Taifa
ipasavyo kwa kukuza vipato vya wananchi wanaojishughulisha na shughuli za
madini lakini kubwa zaidi ni kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
“Mchango wa Madini
katika Pato la Taifa bado kwa sasa ni asilimia 4.2 tu. Hii ni ndogo sana.
Tunaamini kuwa ikiwa sekta hii itasimamiwa vizuri, mchango wake unaweza kufikia
asilimia 10 na kuendelea,” alisema Nyongo.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri Biteko alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa
dhati kuhakikisha madini yanayopatikana Tanzania, hususan Tanzanite,
yanawanufaisha watanzania zaidi kuliko nchi nyingine yoyote kwani yanapatikana
nchini tu. “Tumechoka kuona madini yetu wenyewe yananufaisha mataifa mengine
zaidi yetu, nasi kuambulia kipato kidogo sana kisichostahili. Hili
tutalisimamia kwa nguvu zetu zote na tunaamini inawezekana,” alisema.
Kauli hiyo ya Naibu
Mawaziri ilikuja kufuatia vyama hivyo vya wachimbaji na wafanyabiashara ya
madini kuwasilisha taarifa zao katika mkutano huo; ambapo walieleza kuwa moja
ya changamoto kubwa wanayoomba Serikali ifanyie kazi ni kubadili kanuni katika
Sheria ya Madini inayoelekeza kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya
kuyasafirisha nje ya nchi.
Akiwasilisha taarifa
husika kwa niaba ya wanachama wa TAMIDA, Mwenyekiti wake, Sammy Mollel alisema
kuwa kumekuwa na mkanganyiko kuhusu maelezo ya kanuni hiyo inayohusu uongezaji
thamani madini nchini.
“Sisi tunaamini
Kanuni hiyo inalenga madini ya metali na ya viwanda lakini siyo madini ya vito.
Madini ya vito yakikatwa, yanapungua thamani hivyo tunaomba Serikali itufikirie
katika hili.”
Hata hivyo, Naibu
Mawaziri Biteko na Nyongo, wakitolea ufafanuzi zaidi suala hilo, walisema kuwa
Wizara iko katika hatua za mwisho kukamilisha Mwongozo maalum utakaobainisha
kila aina ya madini yanapaswa kuwa katika hali gani au kuongezwa thamani kwa
kiasi gani kabla hayajatolewa kibali cha kuyasafirisha nje ya nchi. “Mwongozo
huo tutautoa hivi karibuni maana kwa sasa tunaukamilisha.”
Katika hatua
nyingine, Nyongo na Biteko walisisitiza ushirikiano baina ya Serikali na wadau
hao wa sekta ya madini katika kufanikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini
hivyo kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutokana na biashara hiyo.
“Tunaomba sana mtupe
ushirikiano. Tukishirikiana tutafanikiwa. Tuleteeni majina ya wanaotorosha
madini pamoja na taarifa nyingine mbalimbali zinazohusu sekta hii ambazo
mnahisi zinaweza kutusaidia kudhibiti suala husika.”
“Mkiona
tunashughulika katika kipindi hiki cha mpito msidhani Serikali inawachukia.
Naomba niwahakikishie kuwa Rais John Magufuli anawapenda sana wachimbaji.
Lakini anachukia sana anapoona wachimbaji wanasaidia kufanya haya madini
yanufaishe nchi nyingine. Sasa mtusaidie.”
Aidha, Naibu Mawaziri
Nyongo na Biteko waliwahakikishia wachimbaji na wafanyabiashara hao wa madini
kuwa, hoja zote walizoziwasilisha zitafanyiwa kazi na Serikali.
“Tumesikia hoja zote
mlizowasilisha. Ni nzuri. Tumezichukua. Hii ni pamoja na suala la
ushirikishwaji ambalo mmeliongelea. Sisi tutaendelea kushirikiana nanyi.”
Mkutano huo
ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Gabriel Daqarro, Mbunge wa
Simanjiro James Ole Millya, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Adam
Juma pamoja na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini.
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo akizungumza katika Mkutano na viongozi wa Chama cha
Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini
Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.
Naibu Waziri wa
Madini Doto Biteko akizungumza katika Mkutano na viongozi wa Chama cha
Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini
Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.
Mbunge wa Simanjiro
James Ole Millya, akizungumza katika Mkutano baina ya Naibu Mawaziri wa Madini
Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyabishara
wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania
(FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.
Mwenyekiti wa Chama
cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sammy Mollel, akizungumza
katika Mkutano baina ya Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto
Biteko pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyabishara wa Madini Tanzania
(TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mkutano
ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.
Baadhi ya
wafanyabiashara na wachimbaji wa madini nchini, wakizungumza katika Mkutano
baina ya Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na
viongozi wa Chama cha Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha
Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka
huu Arusha.
No comments:
Post a Comment