Na Veronica Simba, Longido
Serikali
imewaahidi wakazi wa Kata ya Mundarara katika Wilaya ya Loliondo kuwa
itahakikisha madini ya Ruby ambayo yanapatikana katika eneo hilo yanaendelea
kuwanufaisha na siyo kuwadidimiza.
Ahadi
hiyo ilitolewa jana, Aprili 13 na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na
Dotto Biteko baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaojishughulisha na uchimbaji
wa madini hayo na kisha kuzungumza na wananchi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Nyongo na Biteko waliwataka wananchi wa Mundarara kuondoa
hofu kuwa neema ya madini hayo yanayopatikana katika maeneo yao haitawanufaisha
tena kutokana na kile wanachodai kuwa sheria mbalimbali zilizowekwa na Serikali
zinasababisha kupungua kwa Soko lake.
Akizungumza
na wananchi hao, Naibu Waziri Biteko aliwaambia kuwa, Serikali kupitia Wizara
ya Madini inaandaa mwongozo maalum utakaobainisha utaratibu unaopaswa kutumika
katika biashara ya kila aina ya madini hapa nchini ili yaweze kuwanufaisha wananchi
na Taifa ipasavyo.
“Nia
ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha rasilimali zote zinazopatikana
nchini yakiwemo madini, zinalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili. Kwa
muda mrefu tumekuwa tukiibiwa sana na watu wengine kunufaishwa na rasilimali
zetu wenyewe ilhali sisi tunazidi kuwa maskini. Sasa tumeamua kuwa hatutaki
kuibiwa tena,” alisisitiza.
Akifafanua
zaidi, Biteko alisema kwamba, mwongozo huo unaoandaliwa na Serikali utasaidia
hata wananchi wanaozungukwa na Migodi ya Madini kunufaika zaidi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi hao wa Mundarara kuwa na
subira wakati Serikali ikishughulikia hoja zao walizoziwasilisha.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuziba mianya yote ya wizi wa
rasilimali madini hivyo alitoa wito kwa wote waliozoea kufanya biashara hiyo
kwa udanganyifu kuacha mara moja vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Mnapaswa
kufanya biashara iliyo safi. Msiiibie Serikali maana tunahitaji kodi na tozo
stahiki kutoka biashara hiyo ili zituwezeshe kuwaletea wananchi maendeleo
ikiwemo kujenga barabara, hospitali, shule, huduma za maji safi na nyinginezo.”
Awali,
akiwasilisha taarifa kwa Naibu Mawaziri kwa niaba ya wananchi wa Mundarara,
Diwani wa Kata hiyo, Alais Mushao alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto
kadhaa, kubwa ikiwa ni kushuka kwa soko la madini ya Ruby, hali inayosababisha
kushuka kwa kipato chao hivyo kurudisha nyuma maendeleo.
“Kutokana
na idadi ya wanunuzi wa Ruby kuzidi kupungua siku hadi siku, inasababisha wao
kujipangia bei wanayoitaka na hivyo sisi kutonufaika,” alisema Mushao.
Aliongeza
kuwa, kutokana na hali ya uasili wa madini ya Ruby kuwa madogomadogo
husababisha kupasuka na kupukuchika. Kufuatia hali hiyo, madini hayo
yanapokatwa ili kuyaongezea thamani, yanazidi kupoteza uasili na ubora wake
hivyo kushusha zaidi thamani yake.
“Kwa
hivyo, tunaiomba Serikali iondoe madini haya katika orodha ya madini
yanayotakiwa kukatwa ili turuhusiwe kuyauza kama yalivyo, Soko lake lipande
nasi tuendelee kunufaika,” alisema Diwani Mushao.
Wakihitimisha
Mkutano huo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko, walipongeza uhusiano mzuri uliopo
kati ya Mwekezaji wa Mgodi na wananchi hao ambao walisema ni wa mfano wa
kuigwa.
Ilielezwa
kuwa pamoja na kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kata husika,
Mwekezaji huyo amewaruhusu wananchi kuchukua na kuchekecha udongo kutoka
Mgodini pasipo kuwalipisha chochote.
Naibu Mawaziri wa Madini Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo wakizungumza na wawekezaji wa Mgodi wa Madini ya Ruby katika Kijiji cha Mundarara wilayani Longodo, Februari 13 mwaka huu. |
Sehemu ya eneo kunakochimbwa madini ya Ruby katika Kijiji cha Mundarara, Wilaya ya Longido. |
No comments:
Post a Comment