Na Mohamed Saif
Serikali imeagiza hadi kufikia Machi 5, 2018 Ukaguzi wa Usalama
kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa uwe
umekamilika na machimbo hayo yawe yamefunguliwa ili kuruhusu shughuli za
uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa zianze.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa agizo hilo
Februari 19, 2018 alipofanya ziara kwenye machimbo hayo yaliyoko katika Kata ya
Malengamakali, Wilayani Iringa ili kujionea hali halisi ya machimbo husika
pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao hadi
hapo ukaguzi utakapokamilika.
“Serikali haifurahishwi kuona shughuli za uchumi kwenye eneo
hili la Machimbo ya Nyakavangala zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji
kusimamishwa kutokana na ajali,” alisema.
Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye machimbo
hayo ya Nyakavangala Februari 12, 2018 baada ya kutokea vifo vya
Wachimbaji Wawili Tarehe 30
Januari, 2018 kutokana
na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.
Biteko aliagiza wakaguzi kukamilisha zoezi hilo haraka ili
shughuli za uchimbaji ziendelee na aliwataka wachimbaji hao kuwa na subira
wakati zoezi hilo la tathmini likiendelea ili kuepusha maafa mengine kutokea.
“Mgodi huu hautafunguliwa bila kukamilisha zoezi la ukaguzi
kwahiyo ndani ya wiki mbili kutoka leo Wakaguzi wawe wamekamilisha ili mgodi
uanze kazi na shughuli za uchumi zilizokuwa zikifanyika mgodini hapa zirejee,”
alisema Biteko.
Aidha, Biteko aliwaonya wachimbaji madini nchini kuacha kufanya
shughuli za uchimbaji kwa mazoea badala yake wahakikishe wanafuata sheria na
taratibu za uchimbaji salama ili kuepusha ajali inayopelekea kuzorota kwa
shughuli za kiuchumi baada ya migodi husika kufungwa.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuifungia migodi
inayosababisha ajali na hivyo aliwasisitiza wachimbaji kote nchini kuhakikisha
wanafuata ushauri wa kitaalam wanaopewa na Maafisa Madini.
"Maisha ya mtu mmoja ni muhimu kuliko shughuli zote za
uzalishaji mgodini, ikitokea kifo kwa sababu ya ajali tunafunga mgodi,"
alisema Biteko.
Sambamba na hilo, Biteko aliwaagiza Wakaguzi wa Migodi
kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya machimbo ili kujionea hali ya
uchimbaji pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji bora na salama kwa wachimbaji
ili kuepusha ajali.
Naibu Waziri Biteko alifanya ziara kwenye machimbo ya
Nyakavangala ili kujionea hatua za kiusalama zilizofikiwa tangu kufungwa kwa
machimbo hayo kufuatia matukio matatu ya ajali yaliyotokea kwa nyakati tofauti
ambayo yalisababisha vifo vya Wachimbaji Wanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa,
Robert Masunya ilielezwa kuwa, tukio la kwanza la ajali lilitokea Juni 12, 2017
na kusababisha kifo cha Mchimbaji Mmoja, la pili lilitokea Novemba 30, 2017 na
kisababisha kifo cha Mchimbaji Mmoja na tukio la tatu lilitokea Januari 30,
2018 na kusababisha vifo vya wachimbaji wawili.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela,
Kamati za Ukinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya ya Iringa na Wataalam kutoka
Wizara ya Madini.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na Wachimbaji Madini wa Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mgodini hapo. |
Baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Nyakavangala Wilayani Iringa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (aliyeshika kipaza sauti) wakati wa ziara yake mgodini hapo. |
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza mara baada ya kukagua moja ya shimo la dhahabu kwenye Machimbo ya Nyakavangala Wilayani Iringa. |
No comments:
Post a Comment