Friday, February 23, 2018

Nyongo asuluhisha mgogoro wa wachimbaji madini Ishokelahela


  • Kamishna Msaidizi Kanda ya Ziwa atoa maagizo mwekezaji alipe fidia
Na Veronica Simba, Mwanza

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefanikiwa kusuluhisha mgogoro baina ya wachimbaji madini wadogo wa vikundi vya Basimbi na Buhunda vilivyopo eneo la Ishokelahela, wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza ambao umedumu kwa miaka Saba.

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kazi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Naibu Waziri Nyongo alikutana na viongozi na baadhi ya wanavikundi vya wachimbaji hao, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda na kuendesha kikao cha usuluhishi huo.

Akitoa maamuzi ya usuluhishi, baada ya kuzungumza nao, Naibu Waziri aliwataka wachimbaji hao, ambao kimsingi hawana leseni na wamevamia eneo la mwekezaji Carlton Kitongo, kuachana na malumbano na waungane pamoja ili waendelee na shughuli za uchimbaji katika eneo ambalo mwekezaji huyo ameamua kuwapatia.

“Mwekezaji amekubali kuwaachia eneo ili muungane na kuchimba kwa pamoja. Hivyo ninawataka make pamoja muelewane na muendelee na shughuli za uchimbaji katika eneo mlilopewa.”

Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa, eneo ambalo moja ya vikundi hivyo walivamia na hawataki kuliachia, haliruhusiwi kufanya shughuli yoyote ikiwemo uchimbaji, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, kwa kuwa ni eneo lililotengwa kwa taratibu za kiusalama (buffer area) kutokana na shughuli za ulipuaji miamba kwa baruti na nyinginezo zinazofanyika Mgodini.

“Kwa sababu hiyo, haiwezekani ninyi kuendelea kuchimba katika eneo hilo kwani sheria hairuhusu,” alisisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji hao na wengine kote nchini, ambao wanachimba madini pasipo kuwa na leseni halali zinazotolewa na Serikali, kuhakikisha wanafanya utaratibu wa kuomba ili wapatiwe leseni na hivyo watambuliwe na Serikali na kuweza kufanya kazi zao kwa Amani.

Alisema kuwa, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuilinda Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inaelekeza watu wachimbe madini kwa tija ili waongeze kipato chao na kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kulipa kodi na tozo nyingine stahiki.

Vilevile, aliwataka wachimbaji madini kote nchini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Katiba zao walizojiwekea, bali muhimu zaidi kufuata sheria ya madini na kanuni zake mbalimbali zinavyoelekeza.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, akiunga mkono maagizo ya Naibu Waziri Nyongo, alisema kuwa umefika wakati kwa wachimbaji wote wa madini kuhakikisha wanakuwa na nakala ya Sheria ya Madini, waisome muda wote na kujikumbusha kuhusu wajibu na haki zao.

Aidha, aliwataka wachimbaji wadogo wenye tabia ya kuvamia maeneo yenye leseni za wawekezaji kuacha mara moja bali wabaki katika maeneo yao na kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Mbunge wa Misungwi Charles Kitwanga, pamoja na kuafiki maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri, aliwataka wachimbaji hao kujenga tabia ya kuheshimu mikataba yao ya kazi ili waweze kufanya kazi katika mazingira yenye amani hivyo kuepuka migogoro.

Akizungumza katika kikao hicho, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina aliwataka wachimbaji wenzake kote nchini kuwa na umoja na kujenga tabia ya kuwajibika.

Awali, akieleza namna Serikali inavyowajibika katika kutetea na kusimamia haki za wachimbaji wadogo, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba alibainisha kuwa hakuna mwekezaji yeyote anayeruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji kabla ya kuwalipa fidia wananchi wenye maeneo ambayo yatakuwa ndani ya leseni yake.

Sambamba na ufafanuzi huo, Mhandisi Samamba alitoa maagizo kwa mwekezaji wa Mgodi wa Isinka, kuhakikisha anamlipa mwananchi mwenye eneo ambalo liko ndani ya leseni yake, Mama Malosha Lutamla kabla ya kuanza kazi kwa Mgodi huo.

Naibu Waziri Nyongo anaendelea na ziara yake katika Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, ambayo ni pamoja na Geita, Kagera na Kigoma.

Mmoja wa wamiliki wa Mgodi wa Dhahabu wa Isinka, Baraka Ezekiel (mwenye shati la mikono mifupi-katikati) akifafanua jambo kuhusu Mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (aliyeshika karatasi-katikati), alipotembelea na kukagua Mgodi huo akiwa katika ziara ya kazi mkoani Mwanza, jana Februari 22, 2018.

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba (kulia) akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kushoto) na wachimbaji wa madini kutoka vikundi mbalimbali, kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda (katikati) jana Februari 22, 2018.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini kutoka vikundi mbalimbali kwa ajili ya kusuluhisha migogoro baina yao. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, jana Februari 22, 2018. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi mkoani Mwanza.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (mbele-kulia), akikagua maeneo ambapo wachimbaji wadogo wa madini wa vikundi vya Buhunda na Basimbi eneo la Ishokelahela wilayani Misungwi wanachimba. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi mkoani Mwanza jana Februari 22, 2018.



Shimo wanalochimba dhahabu wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Basimbi kilichopo eneo la Ishokelahela wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza. Hapa ni wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo jana, Februari 22, 2018.

Sehemu ya umati wa wananchi wa Ishokelahela wakiwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), jana Februari 22, 2018.

No comments:

Post a Comment