Ø Wawataka Watanzania kuondoa hofu
kuhusu manufaa yake
Ø Ujenzi wafikia asilimia 98
Na
Veronica Simba, Mererani
Naibu Mawaziri wa
Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko wamefanya ziara mahali kunapojengwa
ukuta maalum kuzunguka machimbo ya Tanzanite Mererani na kutoa pongezi kwa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kutekeleza shughuli ya ujenzi kwa kasi na
kiwango cha hali ya juu.
Wakizungumza kila
mmoja kwa wakati wake, baada ya kuhitimisha ziara yao katika eneo hilo,
Jumatatu Februari 12 mwaka huu, Naibu Mawaziri hao walisema iko haja kwa
watanzania wote kuiga uzalendo uliooneshwa na wanajeshi hao.
“Mfano tuliouona
kutoka JKT kutokana na uzalendo wao ni fundisho kwa wananchi wote. Vijana wa
JKT wamefanya kazi kubwa. Tumeshuhudia ari yao kubwa ya kufanya kazi kwa
kujitolea. Uzalendo waliouonesha ni mfano wa kuigwa na watanzania wote,”
alisema Nyongo.
Aliongeza kuwa wametembelea
na kujionea wenyewe kazi ya ujenzi inavyoendelea na kuridhika. Akifafanua
zaidi, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Ukuta ulikuwa ujengwe ndani ya miezi
sita lakini katika muda wa miezi mitatu, uko katika hatua za mwisho kukamilika,
jambo ambalo linapaswa kupongezwa na mpenda maendeleo yeyote.
Aidha, Naibu Mawaziri
walipongeza jitihada zilizofanywa na Jeshi hilo chini ya usimamizi wa Kamanda
wa Operesheni Ujenzi wa Ukuta Mererani, Kanali Charles Mbuge, ambazo zimesaidia
kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ujenzi.
“SUMA-JKT wametupa
somo kubwa sana watanzania, kwamba utumiaji wa wakandarasi wanaopandisha bei
hauisaidii nchi. Na katika hili, nina uhakika baada ya muda watu watatoka
mataifa mengine kuja kujifunza hapa kwetu,” alisisitiza Naibu Waziri Biteko.
Kuhusu suala la
Ujenzi wa Ukuta husika kuhofiwa na baadhi ya watu kuwa utaondoa au kupunguza
fursa za wananchi kunufaishwa na madini hayo adhimu, Naibu Mawaziri kwa umoja
wao waliwataka watanzania kuondoa hofu kwani lengo hasa la ujenzi huo ni
kuongeza fursa kwa watanzania na Taifa kwa ujumla kunufaika na siyo kinyume
chake.
“Niwahakikishie
wananchi wa Simanjiro na Tanzania yote kwa ujumla, kuwa Ukuta huu unakwenda
kudhibiti rasilimali yao ya madini ya tanzanite ambayo kwa muda mrefu imekuwa
ikinufaisha mataifa mengine wakati inapatikana Tanzania pekee,” alisema Biteko.
Aliwaomba wananchi wote
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kuhakikisha
rasilimali hiyo inalinufaisha Taifa ipasavyo.
Pamoja na pongezi
hizo kwa JKT, Nyongo na Biteko pia walitoa pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli
kwa kuasisi suala la ujenzi wa Ukuta huo.
“Tunampongeza
Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha Ukuta huu unajengwa kutokana na maagizo yake
aliyoyatoa Septemba 20 mwaka jana ambayo yalipelekea JKT kuanza utekelezaji wa
awali mara moja siku moja baadaye yaani Septemba 21,” alisema Nyongo.
Akifafanua zaidi,
alisema kuwa hivi sasa ujenzi umekamilika katika eneo lote lenye urefu wa
kilometa 24.5 na kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni kukamilisha mambo madogo
madogo yanayolenga kuimarisha zaidi Ukuta huo.
Aidha, Nyongo
aliongeza kuwa kazi iliyobaki kwa Wizara ya Madini ni kuhakikisha inafungwa
mitambo ya kisasa ya ulinzi ili eneo liwe na usalama zaidi. “Vilevile tunataka
hili Geti likianza kufanya kazi tuwakague wanaoingia na kutoka wanaingia na
nini na kutoka na nini. Lengo ni kuimarisha zaidi ulinzi na kulinda rasilimali
yetu ya tanzanite.”
Suala jingine ambalo
Naibu Mawaziri hao walieleza ni kuhusu utoaji wa elimu kwa wananchi ili wajue
utaratibu watakaoutumia kuendesha shughuli zao za madini ndani ya ngome ya
Ukuta huo.
Walisema kuwa, kwa
Kampuni zinazoendesha shughuli zake mahala hapo, zitashirikishwa pia ili
kuangalia namna watakavyotunza Ukuta huo lakini pia ni kwa namna gani Ukuta huo
utumike kulinda shughuli zote za uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake,
Mbunge wa Simanjiro James Millya, ambaye alishiriki katika ziara hiyo,
aliishukuru na kuipongeza Serikali kwa kupigania maslahi ya wananchi wa Jimbo
lake kwa kuhakikisha Ukuta huo unajengwa ili kudhibiti utoroshwaji wa madini ya
tanzanite.
Naye Kanali Mbuge
alitoa rai kwa Taasisi mbalimbali za Serikali kuendelea kuwapatia kazi
mbalimbali JKT kutokana na mfano mzuri waliouonesha kupitia ujenzi wa Ukuta
husika.
“Kupitia ujenzi wa
Ukuta huu, naomba tupewe kazi nyingi. Nadhani mfano wa utendaji kazi wetu
unaozingatia uzalendo wa hali ya juu tumeuonesha. Hapa kazi tu, hakuna maneno,”
alisisitiza Kanali Mbuge.
Akitoa mfano, Mbuge
alieleza kuwa, moja ya eneo ambalo JKT imefanikiwa kuokoa fedha na kupunguza
gharama za ujenzi wa Ukuta ni kutokana na kuwatumia vijana wa JKT ambao
walijitolea kufanya kazi hiyo bure pasipo malipo yoyote. “Tungesema tuwalipe
vijana hawa, basi tungeongeza gharama ya shilingi bilioni 2.6.”
Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro, Zephania Chaula mbali na kupongeza kazi iliyofanyika, alisema kuwa
wamejipanga, kuanzia Februari 15 mwaka huu kuimarisha zaidi ulinzi wakati
wakisubiri ufungwaji wa vifaa vya kisasa vya ulinzi katika Ukuta.
“Simaanishi kwamba
kwa sasa hakuna ulinzi, la hasha, ulinzi upo isipokuwa tunaimarisha zaidi. Hii
itahusisha ukaguzi madhubuti wa kila anayeingia na kutoka, hata kabla
hatujafunga vifaa vya kisasa vya ulinzi zikiwemo Kamera za CCTV.”
Jumla kuu ya gharama
za ujenzi wa Ukuta wa Mererani ni shilingi bilioni 5.6 ambapo kwa mujibu wa
Kanali Mbuge, ujenzi umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilishwa mapema
zaidi kabla ya muda alioutoa Rais.
No comments:
Post a Comment