Na
Rhoda James, DSM
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki mwishoni mwa wiki alikutana na Ujumbe wa Benki ya Dunia jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na kuangalia hatua mbalimbali
zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi ya Madini inayotekelezwa kupitia Mradi
wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki hiyo
kwa kushirikiana na Serikali.
Pamoja na mambo
mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Waziri Kairuki aliitaka Benki ya
Dunia kuona namna ya kuwaendeleza Wataalam wa Sekta ya Madini ili kuwezesha
uwepo wa Watalaam wa kutosha hususan katika masuala ya Uthaminishaji wa Madini
ya Almasi, tanzanite na madini mengine ya vito na pia masuala ya uongezaji
thamani madini kwa ujumla.
Pia, alishauri
umuhimu wa kuboreshwa kwa Mtandao wa Huduma za Leseni kwa Njia ya Mtandao (Online Mining Cadastre) ikiwa ni pamoja
na kuunganisha mtandao huo na Mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Wakala wa Jiolojia
Tanzania (GST) ili taarifa zote zinazohusu madini na mapato yatokanayo na
madini ziweze kupatikana kupitia mtandao huo.
Vilevile, aliishauri
Benki hiyo kuhusu uuzwaji wa Madini ya Almas kwa njia ya Mnada kama vile inavyofanyika
kwa Madini ya Tanzanite, lengo likiwa ni kuwezesha Serikali kunufaika na madini
hayo.
Hivyo, Waziri Kairuki
amewataka wawekezaji kutokuwa na hofu kwani mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha
kuwa Serikali inanufaika ipasavyo kutokana na rasilimali zake za madini. Aidha, alisema kwamba, nia ya Serikali
kuhusu kuvutia wawekezaji iko palepale ilimradi wazingatie Sheria na taratibu.
Vilevile, Waziri
Kairuki alieleza kwamba, ni vema Benki ya Dunia ikaangalia namna bora ya
kuhakikisha madini yote ya Tanzanite yanayouzwa nje ya nchi yanakuwa na Hati ya
Uhalisia inayoonyesha chanzo cha madini hayo suala ambalo litawezesha Taifa
kupata mapato stahiki kutokana na rasilimali hiyo.
Vievile, Waziri Kairuki
alizungumzia suala la udhibiti wa utoroshaji madini na kusisitiza kuhusu kuwepo
na namna bora ya kuzuia utoroshwaji wa madini ya Tanzanite ikiwemo kujulikana kwa
idadi ya wachimbaji wadogo, wa kati, kiasi kinachopatikana na mahali madini
hayo yanapouzwa.
Pia, Waziri Kairuki
aliishukuru Benki ya Dunia kutokana na ushirikiano ambao umekuwepo baina ya Serikali
kwa kipindi chote na kueleza kuwa, Serikali iko tayari kutekeleza miradi husika
kikamilifu kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Naye, Katibu Mkuu
Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila aliiomba Benki ya Dunia kuleta
Wataalam wa madini nchini ili waweze
kutoa mafunzo katika vituo vya Madini nchini ikiwemo Chuo cha Madini Dodoma
(MRI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuzalisha wataalam zaidi katika
Sekta hiyo.
Kwa upande wake,
Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa, tayari
Serikali imefanya jitihada kadhaa za kuanzisha mfumo wa utoaji wa leseni kwa
njia ya Mtandao. Aliongeza kuwa, kinachotakiwa sasa ni kuimarisha zaidi mfumo
huo ili taarifa zote zinazohitajika na umma zinazohusu madini na mapato ya kodi
na mrabaha ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa uhakika.
Aidha, Kamishna
Mchwampaka aliiomba Benki ya Dunia kukijengea uwezo zaidi Kituo cha Jemolojia
Tanzania (TGC) kilichopo jijini Arusha ili kiweze kutoa mafunzo ya Utambuzi wa
madini na Uongezaji thamani kwa viwango vya Kimataifa.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bella Bird alisema zipo fursa nyingi kwa
Sekta ya madini na hivyo kuiomba Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa inatumia
fedha zilizopo katika miradi husika na kwa wakati.
Aidha, alishauri
Tanzania kujifunza kutoka nchi ya Ethiopia kuhusu namna ya kudhibiti Wachimbaji
Wadogo wa madini ya dhahabu kwa kuwa, nchi hiyo unao mfumo bora Barani Afrika.
Pia, alisisitiza
kuhusu umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za madini nchini.
No comments:
Post a Comment