Mohamed Saif
Serikali
imewakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya
madini nchini.
Waziri
wa Madini, Angellah Kairuki ametoa wito huo Novemba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam
alipokutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wang Ke na ujumbe
alioambatana nao Wizarani kutoka kwenye Ubalozi huo ili kujadiliana masuala
mbalimbali ya madini ikiwemo fursa za uwekezaji.
Waziri
Kairuki alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na
hivyo zipo fursa lukuki za uwekezaji ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za nchini
China kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Rasilimali
za madini ni nyingi na hivyo zipo fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa na
kampuni za China na wakati huo huo kuchangia katika uchumi na pato la Taifa kwa
ujumla,” alisema Waziri Kairuki.
Waziri
Kairuki vile vile alisema yapo maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kushirikiana
na Serikali ambapo alitaja baadhi yake kuwa ni uchimbaji wa madini kwa kushirikiana
na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), tafiti za utambuzi wa maeneo yenye
madini kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo cha Madini
(MRI).
Aidha,
aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa
thamani kabla hayajasafirishwa ili kukuza uchumi wa Taifa na wakati huo huo, kuongeza
mapato ya Serikali na kuzalisha ajira zaidi.
“Madini
yakiongezwa thamani hapa nchini, faida zitakazopatikana ni nyingi na ni kubwa
ikiwemo ajira lakini pia mapato nayo yataongezeka kwa kuelewa thamani halisi ya
madini husika,” alisema Waziri Kairuki.
Ili
kufikia dhamira hiyo ya uongezaji thamani wa madini, Waziri Kairuki alisema
Serikali ipo katika hatua za kuwapata wawekezaji mahiri wa kujenga viwanda vya
kuyeyusha na kusafisha (smelting and refining) madini na alisema kuwa zipo
baadhi ya kampuni kutoka China ambazo pia zimeonesha nia.
Mbali
na hilo, Waziri Kairuki alisema Serikali imelenga kuwa na minada ya madini
mbalimbali nchini na kwamba tayari upo mnada wa madini ya Tanzanite lakini
lengo ni kuwa na minada pia kwa aina nyingine za madini ikiwemo Almasi na hivyo
aliwakaribisha wafanyabiashara kutoka China kushiriki katika minada hiyo.
“Sasa
hivi tunaelekea kwenye mnada wetu wa Tatu wa madini ya Tanzanite, tunawakaribisha
kushiriki,” alisema Kairuki.
Alisema
baada ya kufanikisha uanzishwaji wa minada itakayofanyika hapa nchini, katika
siku za baadaye Serikali itaangalia uwezekano wa kuanzisha mnada kwa njia ya
mtandao ambayo itamuwezesha mnunuzi kununua madini huko huko aliko kwa njia ya
mtandao.
Vilevile,
Waziri Kairuki alimuomba Balozi Ke kupitia ubalozi huo kuendeleza programu yake
ya kuwajengea uwezo Watanzania kupitia masomo ya muda mfupi na mrefu hususan
wafanyakazi kwenye Sekta ya Madini kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Uthaminishaji
wa madini, Jiolojia, Jemoloji, Uongezaji thamani, Uhandisi migodi na Usimamizi
wa Sekta ya Madini ili kuwa na wataalam wengi wenye uwezo mkubwa.
Aidha,
Waziri Kairuki alimpongeza Balozi Ke kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa kwanza
mwanamke kuiwakilisha China nchini Tanzania na kumhakikishia ushirikiano wa
dhati.
Kwa
upande wake Balozi Ke alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwaletea
wananchi wake maendeleo endelevu.
Alisema
Serikali ya China itaendeleza ushirikiano wa karibu na wa dhati na Serikali ya
Tanzania hususan kwenye Sekta ya Madini ili kuhakikisha sekta hiyo inaleta tija
iliyokusudiwa kwa Taifa.
Alisema
kampuni mahiri nyingi kutoka China tayari zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta
ya Madini na ziko tayari kuja kuwekeza Nchini.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (wa pili kutoka kulia) akijadiliana jambo na ujumbe kutoka Ubalozi wa China nchini ulioongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke (katikati). |
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
(kulia) akiagana na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke mara baada ya
kumalizika kwa majadiliano.
|
No comments:
Post a Comment