Monday, January 22, 2018

Wanaodai fidia Nyamongo wahakikishiwa kulipwa

Na Mohamed Saif,

Serikali imewahakikishia Wananchi wa Tarime wanaostahili kulipwa fidia na Mgodi wa North Mara uliopo wilayani humo ambao walifanyiwa tathmini kuwa watalipwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema hayo Desemba 28, 2017 wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Matongo Wilayani Tarime kwenye mkutano na wananchi na wachimbaji wadogo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo hayo walimueleza Naibu Waziri malalamiko mbalimbali ikiwemo suala la ulipaji wa fidia, ajira, mahusiano duni na mgodi na mgodi kushindwa kununua bidhaa zinazozalishwa na wananchi wa maeneo hayo.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Nyongo aliuagiza mgodi huo wa North Mara kuhakikisha unawalipa wananchi fidia wanayostahili. “Haiwezekani mmefanya tathmini halafu baadaye mnageuka kwamba hamtolipa, ubabaishaji wa aina hiyo haupo maana mlikua mmekwisha waandaa wananchi kisaikolojia kwamba mtawalipa,” alisema.

Kwa upande mwingine aliwaonya wananchi wanaofanya udanganyifu kuacha tabia hiyo mara moja kwani kufanya hivyo kunasababisha malipo ya fidia kuchelewa kwa wananchi wanaostahili.

“Hapa nimeelezwa tathmini ya kwanza ilikua na kiasi kidogo cha fidia kilichokuwa kinadaiwa tofauti na tathmini ya mara ya pili na hapa inaonekana kuna baadhi yenu wamefanya udanganyifu,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwatambua waliofanya udanganyifu ili kuharakisha zoezi la ulipaji wa fidia kwa mujibu wa sheria na makubaliano.

“Tathmini ya mara ya pili imeonekana ina kiwango kikubwa, tunaomba ushirikiano wenu kuwabaini waliojiongeza ili zoezi la ulipaji fidia likamilike kwa wakati bila kuwepo udanganyifu,” aliagiza Naibu Waziri Nyongo.

Akizungumzia suala la ajira, Naibu Waziri Nyongo aliuagiza mgodi huo kuhakikisha unatoa kipaumbele kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi na hapohapo aliwaasa wananchi watakaonufaika na ajira hizo kufanya kazi kwa uadilifu.

“Ajira zitolewe kwa wenyeji wenye sifa na nyie ndugu zangu mkipewa kazi fanyeni kwa uadilifu, msiwaharibie wengine wenye nia ya kufanya kazi,” alisema Nyongo.
Kuhusu suala la manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wenyeji, Nyongo alisisitiza mgodi kutumia huduma na bidhaa zinazozalishwa na wenyeji wa hapo jambo ambalo alisema likifanyika kwa weledi litachangia katika uboreshaji wa mahusiano baina ya pande hizo mbili.

Aidha, alitoa rai kwa Halmashauri kuwa fedha wanazopokea za ushuru wa huduma (service levy) kutoka mgodini hapo ambazo zinatakiwa kuleta maendeleo hapo Nyamongo zirudishwe hapo kufanya maendeleo.

“Halmashauri isimamie vema ili kupata ushuru wa huduma kwa kiasi kinachostahili kutoka kwenye mgodi kwa ajili ya maendeleo,” aliagiza Nyongo.

Naibu Waziri Nyongo alisisitiza suala la uboreshaji wa mahusiano, umuhimu wa kutii na kufuata sheria, kuepuka vurugu, amani, usalama na upendo na vilevile mgodi kuachia maeneo ambayo hayafanyiwi kazi kwa ajili ya uchimbaji mdogo. 

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemamba Wilayani Tarime wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) akizungumzia masuala yanayohusu Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ikiwemo ulipaji wa fidia na  suala la ajira kwenye mgodi huo.


Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyabichane, Kata ya Matongo Wilayani Tarime wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) akizungumzia masuala yanayohusu Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ikiwemo mahusiano, ulipaji wa fidia na  suala la ajira kwenye mgodi huo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwapungia mkono wananchi wa Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Matongo Wilayani Tarime mara baada ya kuwasili kijijini hapo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wanaozunguka Mgodi wa North Mara  na wachimbaji wadogo kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kutafuta ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment