Na
Mohamed Saif,
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mining uliopo
katika Kijiji cha Kataryo Mkoani Mara kukaa pamoja na Serikali kujadili tofauti
zilizopo ili kuruhusu mgodi huo kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Alitoa agizo hilo
Desemba 28, 2017 kwenye mkutano na wananchi katika Kata ya Tegeruka kufuatia ombi
kutoka kwa mmoja wa Wakurugenzi wa mgodi huo, Mahuza Nyakirang’ani pamoja na wananchi waliokuwa wakifanya kazi
kwenye mgodi huo na wananchi wa maeneo ya jirani na mgodi waliokuwa wakinufaika
na mgodi kwa namna mbalimbali la kuruhusu uzalishaji uendelee.
Alisema anatambua
umuhimu wa mgodi huo kwa wamiliki na wananchi kwa ujumla na hivyo ipo haja ya
kukaa pamoja kujadili tofauti zilizosababisha kusimamishwa kwa uzalishaji
katika mgodi huo ili uendelee na uzalishaji.
Alisema uangaliwe
uwezekano wa kuruhusu uzalishaji uendelee ili wananchi waliokuwa wameajiriwa mgodini hapo waendelee na ajira
zao huku majadiliano yakiendelea kufanyika.
“Kama mlivyonieleza
kuna baadhi yenu mlikua mkifanya kazi kwenye mgodi lakini tangu mgodi
usimamishwe uzalishaji nanyi hamna kazi, kwahiyo ni vyema wakati mazungumzo
yanaendelea na mgodi ukawa unazalisha ili waliokosa ajira warudi kazini,”
alisema.
Aidha, akizungumza
kwa niaba ya wananchi waishio maeneo jirani na mgodi, Elizabeth Masabu ambaye
ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kataryo alimueleza Naibu Waziri Nyongo kuhusu uhusiano baina ya
mgodi na wananchi na pia kumuomba kuingilia kati masuala mbalimbali ikiwemo ajira
kwa wananchi wa maeneo husika, fidia, utunzaji wa mazingira na migogoro na
mgodi.
Masabu aliongeza kuwa
waliingia mikataba ya kirafiki na mgodi huo ambao alisema kuna makubaliano
ambayo hayajafanyika na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuwasaidia kuhakikisha
mgodi huo unarejea makubaliano.
Akijibu hoja za
wananchi hao, Nyongo aliuagiza mgodi kuhakikisha unaingia mkataba wa kisheria
wa uwajibikaji kwa jamii (corporate
social responsibility) ili Serikali ya Kijiji iweze kujipatia haki yake kwa
mujibu wa makubaliano ya mkataba.
Aliuagiza mgodi huo
kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wa maeneo ya jirani kwa kazi
wanazoziweza na wakati huohuo aliwaasa wananchi watakaonufaika na ajira wafanye
kazi kwa uadilifu.
Kwa upande wake Nyakirang’ani alimuahidi Naibu Waziri Nyongo kwamba mgodi
huo utaendelea kuboresha mahusiano na jamii na kwamba watatekeleza maagizo yake
kwa wakati ikiwemo suala la ulipaji wa fidia.
No comments:
Post a Comment