Na Mohamed Saif, Singida
Wachimbaji
wa Madini ya Jasi Mkoani Singida wametakiwa kufanya shughuli zao kwa uaminifu
ili kujihakikishia soko la uhakika.
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa wito huo Desemba 11, 2017 Wilayani
Manyoni mara baada ya kuzungumza na Wachimbaji wa madini hayo Mkoani Singida
wakati wa ziara yake kwenye maeneo yenye uchimbaji wa madini ya Jasi.
Wachimbaji
wa Madini hayo Mkoani Singida, walimueleza Naibu Waziri Nyongo changamoto
mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika.
Mara
baada ya wachimbaji hao kuelezea changamoto zinazowakabili, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Itigi, Ali Minja alimueleza Naibu Waziri Nyongo kwamba tatizo la
soko la Jasi kutoka Singida linasababishwa na wachimbaji wenyewe kwa
kuchanganya madini hayo na udongo.
Alisema
wakati mwingine wachimbaji wenyewe wanasababisha kupotea kwa soko, kwani
mnunuzi akinunua madini yaliyochanganywa na udongo hawezi kurudi tena kununua.
“Baadhi
ya wachimbaji wa Jasi Mkoani hapa sio waaminifu kwani wanachanganya madini na takataka
ikiwemo udongo, na hii inakimbiza wanunuzi,” alisema.
Kufuatia
hali hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliwaasa wachimbaji hao kuwa wakweli kwa kufanya
shughuli zao kwa uadilifu na ubunifu mkubwa wa utafutaji wa masoko ili kuvutia
wanunuzi wengi zaidi na hivyo kujiongezea kipato.
Alisema
mafanikio hayawezi kupatikana kama wachimbaji watafanya shughuli zao kwa
ulaghai na aliwataka kuacha kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato ikiwemo hiyo
ya kuchanganya Jasi na takataka ambayo alisema imewasababishia kukimbiwa na
wanunuzi.
“Tukitumia
madini haya vizuri huku tukiongeza ubunifu, tutafanikiwa kufikia malengo
tuliyojiwekea; vinginevyo tutaendelea kulalamika,” alisema.
Aliongeza
kwamba Serikali itafanya jitihada za kutangaza Madini ya Jasi yanayochimbwa
nchini na kuwataka wachimbaji wa madini hayo kuhakikisha wanazingatia suala la
ubora unaotakiwa Kimataifa.
“Ninawahakikishia
tutawatafutia soko mahala popote Duniani, ili kuhakikisha mnanufaika na madini
haya mnayochimba ila mkumbuke uaminifu ni muhimu,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aidha,
aliongeza kwamba Serikali inakaribisha wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye
biashara ya Madini ya Jasi ikiwemo ujenzi wa viwanda vinavyotumia Madini ya
Jasi kama malighafi ya kutengenezea saruji na bidhaa mbalimbali kama mapambo ya
majumbani na chaki.
Naibu
Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida kwa ziara ya siku tatu ya kutembelea shughuli
za uchimbaji wa Madini mkoani humo na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini
changamoto zinazowakabili kwa lengo la kutafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment