Na Mohamed Saif,
Serikali
imewataka wanufaika wa ruzuku ambao hawakuitumia kama ilivyokusudiwa warejeshe
fedha walizopatiwa mara moja na vyombo husika vihakikishe waliohusika
kuidhinisha wanawajibishwa.
Agizo
hilo limetolewa Desemba, 12, 2017 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Mkoani
Singida wakati wa ziara yake ya kutembelea Migodi ya Dhahabu kwa ajili ya
kujionea shughuli zinazoendelea na kuzungumza na wachimbaji.
“Aliyenufaika
na ruzuku na hakufanya lolote, arejeshe mara moja fedha hiyo na aliyehusika
kuwapatia ruzuku watu hawa hali yakuwa anaelewa hawakuwa na dhamira ya
kuendeleza uchimbaji nae achukuliwe hatua,” aliagiza Nyongo.
Agizo
hilo linafuatia malalamiko ya wachimbaji wadogo ambao hawakunufaika na mpango huo
wa ruzuku ambapo walimueleza kwamba wapo baadhi ya watu wasiostahili lakini
walipatiwa ruzuku.
Naibu
Waziri Nyongo alisema anampongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa
kusimamisha utoaji wa ruzuku kwani imeshindwa kufikia matarajio yaliyokusudiwa.
Alisema
Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku
kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini baada ya kubaini kwamba imeshindwa
kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.
Nyongo
alisema dhamira ya Serikali ya kutoa ruzuku ilikuwa ni kuhakikisha wachimbaji
wadogo wa madini nchini wanaweza kuendeleza machimbo yao kwa kufanya shughuli
zenye tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.
Hata
hivyo alisema dhamira hiyo haikuzaa matunda yaliyokuwa yamekusudiwa kwani imedhihirika
kwamba ruzuku iliyotolewa haikuwanufaisha
walengwa kama ilivyotarajiwa badala yake ilinufaisha watu wachache tofauti na
ulivyokuwa mpango mzima wa utoaji wake.
“Wapo
wachimbaji wachache ambao walifanikiwa kupata ruzuku na waliweza kuendeleza
migodi; japo hawa ni wachache tofauti na malengo ya Serikali,” alisema Naibu
Waziri Nyongo.
Mbali
na hilo, alisema baadhi ya wachimbaji wadogo walipewa ruzuku na walichimba
lakini hawakufanikiwa kwani walichimba kwa kubahatisha bila kuwa na elimu ya
kutosha ya kutambua uwepo wa mashapo katika maeneo yao.
Kwa
kuliona hilo, Nyongo alisema Serikali ipo katika majadiliano na Vyama vya
Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kuona namna ambavyo wanaweza kuwa na
uchimbaji wenye tija.
Alieleza
kwamba Wizara ya Madini kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo katika umoja wao wameona
ipo haja ya kuwasaidia kufanya utafiti kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania
(GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili waweze kutambua maeneo yenye mashapo
na hivyo kuepukana na uchimbaji wa kubahatisha.
“Wachimbaji
wengi wanafanya uchimbaji kwa kubahatisha na ndiyo maana wapo wengine ambao
wanakimbilia kwenye imani za kishirikina. Hii yote ni kukosa elimu, ya utambuzi
wa maeneo sahihi,” alisema.
Kwa
upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini
Tanzania (FEMATA), John Bina alisema wanaunga mkono jitihada za Serikali katika
kuhakikisha wanakuwa na uchimbaji wenye tija.
Hata
hivyo alisema changamoto inayowakabili wachimbaji wadogo walio wengi ni ukosefu
wa elimu ya utambuzi wa maeneo sahihi yaliyo na mashapo na kwamba msaada wa
Serikali wa kufanya utafiti utawasaidia kufanya uchimbaji wenye faida.
No comments:
Post a Comment