Na Mathias Canal,
Shinyanga
“Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017
inataka kurudisha uchumi wa madini kuwa uchumi fungamanishi kwa sekta nyingine.
Hatuwezi kuwa na Mgodi ndani ya nchi ambao ajira zote zinapelekwa nje ya nchi
kupitia huduma mbalimbali. Unaweza kuagiza bidhaa za kila aina kutoka nje ya
nchi lakini huwezi kuagiza ajira za wananchi wako zitoke nje kuja ndani, kamwe
haiwezekani.”
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri
wa Madini Doto Biteko tarehe 3 Februari 2018, wakati akizungumza na Uongozi wa
Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo alisisitiza viongozi wa serikali
katika maeneo yao kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini.
Biteko alisema kuwa, usimamizi
madhubuti wa Sheria na taratibu zilizowekwa ni sehemu imara na makini
itakayowanufaisha watanzania ambapo watakuwa wamemuunga mkono kwa vitendo Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amedhamiria
kuhakikisha kuwa watanzania wananufaika kupitia rasilimali zao.
“Kanuni ya madini ya
mwaka 2018 imeelekeza kuwa mgodi wowote unapoanza asilimia 100% za watoa huduma
za chakula wanapaswa kuwa watu wa wananchi wa Tanzania, Pia huduma za ulinzi
kwa asilimia 100% zinapaswa kutolewa na kampuni za ndani. Hivyo wataalamu wa
sekta ya madini ni lazima kusimamia Kanuni hizo kwa usahihi,”aliongeza.
Biteko aliongeza kuwa, kampuni ya
kigeni inaweza kufanya huduma hizo lakini ni lazima iingie ubia na wananchi wa
Tanzania na kanuni hizi serikali imeziweka kwa makusudi kabisa ikiwa na mtazamo
wa kuwanufaisha wananchi kupitia rasilimali zao.
Biteko alisema kuwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ndicho kimeingia mkataba na wananchi katika kuwatumikia kwa
usimamizi madhubuti kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 hivyo,
viongozi wa CCM wanapaswa kusimamia vyema serikali ili kuongeza tija katika
utendaji.
Aliongeza kuwa, sambamba na CCM kuisimamia
vyema serikali pia aliwataka watendaji wote wa serikali kuwa na umoja katika
utendaji wao kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali madini huku akitoa onyo Kali
kwa watendaji wa serikali, Viongozi, vyama vya siasa na wananchi kujihusisha na
rushwa kwani kufanya hivyo ni kuzififisha juhudi za serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Magufuli ya kuwainua wananchi wanyonge ili kila mtanzania
aweze kunufaika na rasilimali zilizopo.
"Ndugu zangu ni aibu mno dhahabu
na madini yetu mengine kuchimbwa nchini lakini yanajenga nchi nyingine, uhakika
wa barabara bado hatuna katika maeneo mengi, maji bado hatuna, sekta ya afya
haijaimarika, Zahanati zina shida lakini pia Karibu kila maeneo hatujajidhatiti
kwa asilimia 100% Kwa hiyo Mhe Dc naomba sana msicheke na mtu yeyote anayecheza
na rasilimali zetu This Must be a Serious business, Mimi najua we have the same
spirit lazima tufanye kazi kwa weledi.
Pia, Naibu Waziri Biteko alimpongeza
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Fadhil Nkulu sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala
Ezekiel kwa kuimarisha juhudi na utendaji kazi katika sekta ya madini kwa
maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kila kiongozi
atapimwa kwa matokeo ya utendaji kazi wake na si kwa cheo chake.
“Waheshimiwa Viongozi, Mhe. Rais na
watanzania watatupima kwa matokeo si kwa nafasi na vyeo vyetu” alisisitiza
Biteko.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo alisisitiza viongozi kusimamia Kanuni na taratibu katika Sekta ya Madini. |
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza wakati wa kikao kazi na
Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga aakiwa katika ziara ya kikazi
mkoani humo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kahama
ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Fadhil Nkulu, wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Madini Doto Biteko alipozuru Wilayani humo kwa ziara ya kikazi.
|
No comments:
Post a Comment