Na Greyson Mwase,
Lindi
Maafisa Madini Wakazi
wa Mikoa Nchini wametakiwa kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa mapato ili kuweza kufikia lengo
lililowekwa na Serikali hivyo Sekta ya Madini kuwa na mchango mkubwa kwenye
ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa
leo tarehe 13 Desemba, 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo kwenye
kikao chake na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi
iliyopo Wilayani Nachingwea mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku
mbili kwenye mkoa huo, yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini
pamoja na kutatua kero mbalimbali.
Naibu Waziri Nyongo
aliyekuwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Mhango alisema
kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya
kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa
sekta nyingine kutokana na makusanyo ya kodi mbalimbali za madini.
“Ninawaagiza maafisa
madini wakazi kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa na Serikali kwenye
ukusanyaji wa kodi mbalimbali zitokanazo na Sekta ya Madini kwa kuwa wabunifu,
na tupo tayari kusaidia pale itakapowezekana,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine,
Nyongo aliwataka maafisa madini kujiridhisha na maeneo yanayoombewa leseni
kabla ya kutoa leseni ili kuepusha
migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wamiliki wa leseni na wananchi
wanaozunguka maeneo ya uchimbaji.
Wakati huohuo
akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye kiwanda cha uzalishaji
wa saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Madini
imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye sekta ya madini na
kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili waweze
kuzalisha zaidi na Serikali kupata mapato yake stahiki.
Aidha, Naibu Waziri
alifanya ziara katika machimbo ya kokoto yanayomilikiwa na kampuni za Drumax Construction
na Said Seff na kiwanda cha kutengeneza
vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya mawe kinachomilikiwa na Shirika la
Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi na kuwahakikishia watendaji wake kuwa
Serikali imejipanga katika kutatua changamoto zinazowakabili ili uwekezaji wao
uwe na manufaa, hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mtaalam kutoka
kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, Victor
Kamuhabwa (wa kwanza kulia mbele) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (wa pili kushoto mbele) namna mfumo wa uendeshaji wa mitambo unavyofanya
kazi kwenye ziara ya Naibu Waziri Nyongo kwenye kiwanda hicho tarehe 13
Desemba, 2018.
Mkurugenzi Mtendaji
wa kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa kokoto ya Drumax Construction kwa
kushirikiana na kampuni inayomilikiwa na Said Seif iliyopo katika Wilaya ya
Masasi mkoani Mtwara, George Tayyar (kulia) akielezea changamoto za kampuni
yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) mara alipofanya
ziara kwenye machimbo hayo.
Mtaalam kutoka kiwanda
cha kutengeneza vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya mawe kinachomilikiwa na
Shirika la Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Mhandisi
Kassari Viater (kulia mbele) akielezea namna mashine ya kukata mawe makubwa
inavyofanya kazi kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele)
kwenye ziara ya Naibu Waziri Nyongo kwenye kiwanda hicho.
Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Lindi, Sophia Omari (kulia) akibadilishana mawazo na Mhandisi Migodi Mwandamizi
kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Aidan Gumbo Mhando
(kushoto) kwenye ziara hiyo.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia zawadi aliyokabidhiwa na mmoja
wa watendaji wa kiwanda cha kutengeneza vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya
mawe kinachomilikiwa na Shirika la Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara, Paulo Gembe (hayupo pichani) mara baada ya kuhitimisha ziara
yake katika kiwanda hicho. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara,
Mhandisi Ephrahim Mushi na kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia
Omari.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya
watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara na Ofisi ya Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi mara baada
ya kumalizika kwa ziara.
No comments:
Post a Comment