Na. Rhoda James, Manyoni
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa
Idris Kikula ameagiza Wakuu wa wilaya inchini kutatua migogoro ya wachimbaji wa
madini inayojitokeza katika maeneo yao ili
kuepusha madhara yatokanayo na ucheleweshwaji wa utatuzi wa migogoro hiyo
inayopelekea migogoro hiyo kufikishwa katika ngazi za juu.
Profesa Kikula ametoa kauli hiyo leo
tarehe 15 October, 2018 wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika wilaya ya
Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza katika kikao hicho,
Profesa Kikula aliwaasa Wakuu wa Wilaya kushirikiana na viongozi wa vijiji,
viongozi wa kata kuelewa vyema vyanzo vya migogoro sehemu za machimbo pamoja na kuitatua.
“Tume ya madini haiwezi kutatua
migogoro yote nchi nzima, lazima tushirikiane katika hilo ili kuwasaidia
wanachi kupata haki yao kwa wakati” alisema Profesa Kikula.
Profesa Kikula aliongeza kuwa, wapo
wenyeviti wa wachimbaji wadogo kila mkoa hivyo fanyeni kazi kwa karibu na hao
viongozi wa wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kutatua migogoro
inayojitokeza.
Aidha, Profesa Kikula alitoa wito kwa
wachimbaji wadogo pamoja na Wakuu wa Wilaya kusoma marekebisho ya sheria ya
madini ya mwaka 2017 na kuielewa ili kuwa
na uelewa wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo,
Profesa Kikula alisema kuwa ni pamoja na kuangalia usalama wa wachimbaji
wadogo, kufuatilia na kujiridhisha na utuzwaji wa kumbukumbu za mapato na tozo
mbalimbali, kujiridhisha endapo wachimbaji wanazingatia uchimbaji salama bila
kuathiri mazingira pamoja na kufuatilia endapo wachimbaji wanajishughulisha na
masuala ya kijamii kama vile kujenga shule, zahanati.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya
madini, Abudulkarim Mruma amewasihi Wakuu wa Wilaya kufatilia taarifa za
wachimbaji wadogo ili kujua leseni ya eneo husika inamilikiwa na nani na je
ameajiri watumishi wangapi jambo litakalosaidia katika kupunguza na kutatua
migogoro itakayojitokeza kwa wakati.
Akizungumzia umuhimu wa utunzwaji wa
kumbukumbu kwa wachimbaji wadogo, Dkt.Athenas
Macheyeki Kamishna wa Tume ya madini aliwasisitiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa wachimbaji
wadogo wanatuza kumbukumbu za uzalishaji na uuzaji ili kujua kiasi sahihi cha
uzalishaji na kilichouzwa ili kwa njia hiyo Serikali ijipatie mapato
yanayostahili.
Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Rahabu
Mwagisa alimshukuru Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Kikula kwa ujio wao
Na kuahidi kuwa watatekeleza kwa
umakini mkubwa suala la kutatua migogoro maeneo ya wachimbaji kwa kushirikiana na viongozi wa madini
waliopo katika maeneo yao pamoja na viongozi wa wachimbaji wenyewe.
Aidha, aliahidi kupitia kwa upya na
kuhakikisha marekebisho ya sheria ya madini ya 2017 ameielewa kikamilifu na
kuifanyia kazi katika shughuli za kila siku ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi
anapata haki yake lakini pia serikali inajipatia mapato yake stahiki.
Mwagisa alikamilisha hotuba yake kwa
kuahidi kuwa ataendelea kusimamia na
kudhibiti suala la utoroshaji wa madini na kuhakikisha kinachopatikana kinauzwa
sehemu maalumu lakini baada ya kumbukumbu kuwekwa sawa na tozo stahiki
zimewasilishwa ipasavyo.
Mashine ya kuchimba na kupakua mchanga wa Jasi
katika mgodi wa Yusufu Kabila ambao ni General Business and Equipment Suppliers
ltd |
Mmiliki wa mgodi wa General Business and Equipment Suppliers ltd, Yusufu Kibila akitoa maelezo kwa Kamishna wa Tume, Dkt. Athanas Macheyeki wa kwanza kushoto na Kaimu Afisa Mkazi wa Singida. |
Muonekano wa Machimbo ya mgodi wa dhahabu wa Muhintiri kijiji cha Muhintiri wilaya ya ikungi |
Muonekano wa madini ya Jasi yakiwa yanawekwa pembeni mwa barabara ikiwa pia ni mali ya Yusufu Kibila mgodi wa General Business and Equipment Suppliers ltd |
Mjumbe wa Mgodi wa Muhintiri akieleza changamoto wanayoipata kwa Kamishna wa Tume, Athanas Macheyeki ( mwenye shati la blue) wengine ni wachimbaji wadogo pamoja na watumishi kutoka Tume ya madini. |
No comments:
Post a Comment