Wednesday, October 10, 2018

Kituo kikubwa cha Kimataifa cha Dhahabu kujengwa Geita-Luhumbi


Na Rhoda James, Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Gabriel Luhumbi amesema kuwa Kituo kikubwa cha kimataifa cha Dhahabu kinatarajiwa kujengwa Mkoani Geita hivi karibu ambapo pamoja na mambo mengine kitawezesha wachimbaji wadogo kupata elimu kuhusu uchimbaji wenye tija.

Hayo yalibainishwa jana  28 Septemba, 2018 na mkuu huyo wa mkoa  wakati alipokuwa  akiwahutubia  Wachimbaji Wadogo  wa Madini katika katika Clinik ya Maonesho  ya  Kwanza ya Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji wa Madini ya Dhahabu yanayoendelea  katika Viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita.

Alisema kuwa, bado idadi kubwa ya watumiaji wa madini ya  dhahabu  wanatoka  nje,  hivyo, hawana budi kufahamu  mahali madini hayo yanapotoka   na kuongeza kuwa, ujenzi wa kituo hicho mkoani humo utawezesha kuyatambulisha zaidi madini hayo na mahali yanapotoka.

Aliongeza kuwa, wachimbaji wadogo wamekuwa wakitumia kemikali za sumu katika shughuli zao na kuongeza  kuwa, uwepo ya Kliniki hiyo utawawezesha kupata   majibu kuhusu ni aina gani ya kemikali zinapaswa kutumika katika shughuli za madini ikiwemo  kemikali sahihi zinazopaswa kutumiwa katika shughuli madini na zipi hazipaswi kutumiwa.

Pia, Luhumbi  aliwataka wachimbaji   wadogo wa madini nchini kubadilika  katika masuala  ya utunzaji wa  fedha zao  wanapouza rasilimali hiyo  kwa kuwa wengine wanazichimbia katika mashimo.

“Anzeni kuweka fedha zenu kwenye mabenki, ni sehemu sahihi ya kuweka fedha zenu na mtapata faida nyingi kwa kuweka huko  fedha zenu alisema Luhumbi.

Vilevile, Luhumbi aliwakumbusha wachimbaji wadogo kuhusu umuhimu wa  kuwa na umoja na hususan wanapopata  maeneo ya kuchimba madini ikiwemo pindi wanapopata dhahabu na kuwaasa kuhusu kuacha ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe kugombea maeneo au madini.

“Ishini kama matajiri, matajiri hawagombanii vitu vidogo vidogo, na nyinyi ni matajiri kwa kuwa nyie ndio mnao uza dhahabu,” alisema Luhumbi.

Pia, Mkuu  huyo wa mkoa alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha kuwa Kituo cha Taasisi ya Jilojia na Utafiti  wa Madini Tanzania  (GST) kinajengwa mkoani ili kuwafikia wachimbaji wengi  kwa urahisi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Machayeki alieleza kuwa, hakuna mchimbaji na wadau wengine wa madini watakaokosa leseni ikiwa  watakidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu.

Aliongeza kuwa, ili mchimbaji mdogo aweze kupatiwa Leseni, ni lazima awe na Plan ya Local Content, na kuongeza kuwa, Tume ya Madini inaandaa mwongozo huo.

Pia, alifafanua kuwa,  kwa upande wa wachimbaji wa  Wakubwa na wa Kati wanatakiwa kufuata Sheria na utaratibu wa  Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Naye, Mjiolojio kutoka Wizara ya Madini, Joseph Ngurumwa alisema kuwa, wachimbaji wanatakiwa kuelewa kwamba Sera ya madini inahimiza  kuhusu pande   zote yani Serikali  na wachimbaji  kufaidika  kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.

Kwa upande wa wachimbaji wadogo, waliiomba serikali iendelee kuwapatia elimu zaidi kuhusu uchimbaji ili kuwawezesha kuwa na  uelewa na hususan masuala ya miamba na mabadiliko yake.

Aidha, wachimbaji hao wadogo waliomba kupata  taarifa za utafiti ikiwezekana  za kuhusu nchi nzima ili  kuwawezesha kufanya shughuli za uchimbaji hata katika mikoa mingine.

Pia, walitoa ombi kwa serikali kuhakikisha wanapata Kituo cha umahiri kwa ajili ya mkoa wa Geita kwa kuwa theluthi ya madini ya dhdhabu nchini inatoka mkoani humo.


Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Machayeki akijibu baadhi ya hoja walizokuwa wameuliza wachimbaji wadogo katika kikao hicho kilichofanyika katika viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita. 

Mjiolojia kutoka Tume ya Madini Geita, Godfrey Keraka akitoa mada kwa wachimbaji wadogo katika viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita. 

Mjiolojio kutoka Wizara ya Madini, Joseph Ngurumwa akiwakilisha mada kwa wachimbaji wadogo katika kikao kilichofanyika mkoani Geita tarehe 28 Septemba, 2018. 

Wachimbaji wadogo wakifatilia mada iliyokuwa ikichangiwa na Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Machayeki wakati wa kikao cha wachimbaji wadogo katika viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita tarehe 28 Septemba, 2018. 

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Gabriel Luhumbi akihutubia wachimbaji wadogo katika viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita tarehe 28 Septemba, 2018

No comments:

Post a Comment