Na Mohamed Saif,
Serikali
imesema inaangalia namna ya kuwasaidia wachimbaji Wadogo wa Madini ili kuwa na
uchimbaji wenye manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema hayo Desemba 15, 20017 alipotembelea
eneo lililokuwa Mgodi wa Resolute Wilayani Nzega Mkoani Tabora.
Nyongo
alisema kuwa Serikali imebaini kwamba uchimbaji Mdogo wa Madini hauleti tija
kwa wachimbaji wenyewe na kwa Serikali hasa ikizingatiwa kuwa mapato yatokanayo
na uchimbaji siyo ya kuridhisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu
wa elimu, taarifa sahihi na vifaa kwa wachimbaji.
“Tumegundua
wachimbaji wadogo walio wengi wanahitaji msaada mkubwa kutoka serikalini ili
wawe na uchimbaji wenye tija, si kwao tu bali kwa Taifa kwa ujumla,” alisema.
Akizungumzia
Mgodi wa Resolute ambao ulisitisha uchimbaji madini tangu Mwaka 2014, Nyongo
alisema wapo wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakivamia na kufanya shughuli za
uchimbaji kwenye mashimo hayo jambo ambalo alisema linahatarisha maisha yao.
Alionya
wavamizi wa maeneo hayo kuacha mara moja, kwani kuendeleza shughuli za
uchimbaji kwenye mashimo yaliyoachwa na Resolute ni kuhatarisha uhai.
“Nimetembelea na nimeona mashimo mengi ambayo yamechimbwa na wachimbaji wadogo lakini
bahati mbaya hayajazingatia utaratibu wa uchimbaji,” alisema.
Aliongeza
kuwa, Mwaka 2016 watu wapatao Sita walifariki baada ya kudondokewa na mwamba wa
mawe kwenye mgodi huo wa Resolute eneo ambalo lilipigwa marufuku ya uchimbaji
kutokana na hatari iliyopo ya kuangukiwa na vifusi.
Aliwaasa
wachimbaji hao kuwa na subira kwani dhamira ya Serikali ni kuwasaidia kuwa na
uchimbaji utakaowaletea manufaa zaidi kuliko namna hiyo ya uchimbaji
wanayoifanya hivi sasa ikiwemo kuwapatia maeneo mazuri na salama yaliyofanyiwa
utafiti na elimu ya uchimbaji sahihi.
Alimuagiza
Afisa Madini Mkazi Tabora, Laurent Mayala kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ya Nzega kuhakikisha wanatembelea eneo hilo mara kwa mara ili
kuepusha maafa.
![]() |
Wananchi na Wachimbaji Wadogo wa maeneo
yanayozunguka uliokuwa mgodi wa Resolute wa Nzega wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).
|
![]() |
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
akizungumza na wananchi na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nhobola wilayani
Nzega Mkoani Tabora (hawapo pichani).
|
![]() |
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akitazama
shimo lililochimbwa na wachimbaji wadogo kwenye eneo lilokuwa Mgodi wa Resolute
wilayani Nzega.
|
No comments:
Post a Comment