- · Ataka Wafanyabiashara kuwekeza Mirerani
Na Zuena Msuya, Manyara
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa agizo
kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kusafirisha nje madini
yaliyoongezwa thamani badala ya madini ghafi ili kutekeleza sheria ya madini ya
mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.
Nyongo aliyasema hayo Desemba 21, 2017, wakati wa
Mnada wa Tatu wa Madini ya Tanzanite uliofanyika katika katika Kijiji cha
Naisinyai, katika mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara na
kushirikisha wafanyabiasha wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumzia mnada huo, Nyongo alisema kuwa kwa
sasa Serikali, inatekeleza Sera ya Viwanda katika kila sekta, hivyo kwa
kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa katika Sekta ya Madini ni vyema madini
yanayosafirishwa nje ya nchi yawe yameongezwa thamani kupitia viwanda vya hapa
nyumbani.
Aidha, aliagiza kuwa Minada yote ya madini
itakayofuata, iwe inauza Madini ya Tanzanite yaliyoongezwa thamani kwa kiwango kikubwa
ili kutimiza matakwa ya sheria ya madini na kuunga mkono Sera ya Serikali ya
uchumi wa viwanda.
Vilevile, aliwahakikishia wafanyabiashara wa
madini ya Tanzanite kuwa serikali imeanza kutazama kero mbalimbali zinazoathiri
ushindani katika kufanya biashara ya madini nchini kwa lengo la kuondoa kero
hizo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wadau
mbalimbali kuwekeza huduma muhimu katika Mji Mdogo wa Mirerani kwa kuwa mji huo
kwa sasa ni kitovu cha biashara ya Madini ya Tanzanite .
Nyongo alisema kuwa, lengo la kuwekeza katika Mji Mdogo wa Mirerani
ni kuwafanya wageni wanaofika katika mji huo wakati wa mnada kutumia fedha zao
kwa kupata huduma mbalimbali na hivyo kuleta maendeleo zaidi kwa wakazi
wanaozunguka mji huo.
“Napenda kutoa wito kwa wafanyabiashara na wadau
wote nchini kuwekeza huduma muhimu
katika Mji wa Mirerani kama vile Hoteli za kisasa, Taasisi za Fedha,Maduka
ya kisasa na huduma nyinginezo ili wageni watakaofika hapa wasipate adha ya kutafuta
huduma hizo nje ya Mirerani badala yake
fedha hizo zitumike hapa,” alisema Nyongo.
Alisisitiza kuwa huduma hizo zikiwepo zitachangia
juhudi za Serikali katika kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za
Uchumi na kutafsiri suala la kunufaisha jamii katika eneo husika kiuchumi (Local Content) kwa vitendo.
Mnada wa Madini ya Tanzanite ulifanyika kwa muda
siku tatu kuanzia Desemba 18-21 2017, ambapo kampuni 60 zilishiriki katika mnada huo kutoka nchi
mbalimbali Duniani zikiwemo U.S.A, Sri Lanka, Hong Kong, India, China Thailand
na wenyeji Tanzania.
![]() |
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
akizungumza wakati wa Mnada wa Madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro.
|
No comments:
Post a Comment