Friday, October 12, 2018

Serikali haitamwonea aibu asiyelipa kodi ya madini-Nyongo


Na Greyson Mwase, Katavi

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini haitamwonea aibu mchimbaji yeyote wa madini atakayekwepa kulipa kodi Serikalini  kwa kuwa ni kinyume na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

Ameyasema hayo leo tarehe 11 Oktoba, 2018 katika  mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli zao katika machimbo ya Reef D, yaliyopo katika kata ya Magamba mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake  katika mkoa huo yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika,  Salehe Mhando,  Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Katavi (KATAREMA), William Mbongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na waandishi wa habari.

Alisema kuwa, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wasio waaminifu wanaokwepa kulipa kodi serikalini hali inayokwamisha  upatikanaji wa huduma nyingine muhimu katika jamii kama vile elimu, maji, barabara.

“Mchimbaji ambaye anakwepa kulipa kodi mbalimbali kama Sheria ya Madini na kanuni zake inavyofafanua ni adui namba moja katika ukuaji wa maendeleo ya nchi, hivyo sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga kuchukua hatua za kisheria nia ikiwa ni kutaka kila mwananchi anufaike na rasilimali za madini kupitia uboreshaji wa huduma mbalimbali,”alisema Nyongo

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka maafisa madini wakazi katika mikoa yote kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwani Sekta ya Madini inatarajiwa mno kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaamini kuwa iwapo Sekta ya Madini itasimamiwa kikamilifu, inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye  ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uimarishaji wa sekta nyingine muhimu.

Aidha, aliwataka maafisa madini nchini kushirikiana na  vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya kwenye zoezi la ukaguzi wa shughuli za madini ili kuongeza tija kwenye  ukaguzi.

Katika mkutano huo mbali na wachimbaji wadogo kumpongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kusikiliza na kutatua changamoto kwenye  shughuli za uchimbaji madini katika mkoa wa Katavi, wachimbaji hao waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahitaji ya mikopo katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, mafunzo kuhusu sheria ya madini na kanuni zake, uchimbaji salama na vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchimbaji wa madini.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo katika eneo hilo, Imso Masumbuko kutoka kikundi cha Kagera Group alisema kuwa wana uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu uchimbaji wa madini  salama pamoja na vifaa vya kisasa ili waweze kuzalisha na kulipa kodi zaidi Serikalini.

Masumbuko mbali na kuainisha changamoto hizo aliiomba Wizara ya Madini kuiomba Wizara ya Nishati ili iweze kufikisha umeme katika machimbo hayo  kupitia Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III)
Alifafanua kuwa, kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme katika eneo lao wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye uzalishaji wa madini kutokana na matumizi ya dizeli hivyo kupata faida kidogo sana.

Naye Karusum Daudi ambaye ni mchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo hilo aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini iangalie uwezekano wa kuwapatia mikopo ili waweze kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi na kusikiliza kero mbalimbali za watumishi ikiwa ni pamoja na kuzitatua.

Pia Naibu Waziri Nyongo alikutana na wachimbaji wadogo wa madini mjini Mpanda lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.
Mbali na kuwasilisha changamoto mbalimbali zilizotatuliwa na Naibu Waziri Nyongo papo hapo  wachimbaji wadogo wa madini walimpongeza Naibu Waziri Nyongo na kumwomba kuendelea na ari ya kusikiliza kero zao na kuzitatua.

Akizungumza katika kikao hicho, Nyongo alisema Wizara ya Madini haitachoka kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini nchini kwa kuwa inataka wachimbe katika mazingira mazuri na kulipa kodi Serikalini.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Reef D, yaliyopo katika kata ya Magamba mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake  katika mkoa huo yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 11 Oktoba, 2018 

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini kutoka machimbo ya Reef D, yaliyopo katika kata ya Magamba mkoani Katavi wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara 
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Reef D, yaliyopo katika kata ya Magamba mkoani Katavi akiwasilisha kero yake mbele ya  Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) 
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akioneshwa mchoro wa ramani ya jengo linalojengwa la Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi na  Mhandisi Andrew Mpangalala kutoka SUMA JKT ( wa kwanza kulia) ambao ndio wajenzi wa jengo hilo katika eneo la Msasani mjini Mpanda mkoani Katavi. 
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi mara baada ya kufanya nao kikao kilicholenga kujadili utendaji kazi.

No comments:

Post a Comment