Ø Awataka watumishi kufanyia kazi maagizo ya Rais
Magufuli
Ø Amshukuru Waziri Kairuki kuwa, amemfundisha Mengi
Na Asteria Muhozya,
Waziri wa
Madini Doto Biteko amekutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini, Taasisi zake
pamoja na Wenyeviti wa Tume ya Madini na Bodi ya Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO), jijini Dodoma, katika kikao ambacho pia kimejadili namna ya
kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli
aliyoyatoa wakati akimwapisha Waziri Biteko kushika wadhifa huo Januari 9, 2019.
Biteko amewataka
watumishi wa Wizara na Taasisi zake ambao
hawayajayasikiliza maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli kuhakikisha kuwa
wanayasikiliza ili kuweka uelewa wa pamoja na kushirikiana katika kutekeleza majukumu
ya wizara kwa lengo la kuhakikisha
kwamba sekta ya madini inaimarika.
“Tuliulizwa dhahabu inauzwa wapi? Basi tusisubiri
tena Rais atuulize inauzwa wapi,” amesisitiza Biteko.
Aidha,
amesisitiza kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja miongoni mwa watumishi wa wizara
katika utekelezaji wa majukumu hayo na kusisitiza kuhusu mabadiliko yanayoonekana
kupitia sekta ya madini ikiwemo kufanya kazi na kuongeza kuwa, “Kinachotuunganisha mahali hapa ni kazi na wala si dini ama jambo lingine,”.
Ameongeza
kuwa, kiu kubwa ya Rais Magufuli ni kuona kuwa watanzania wote wananufaika na
rasilimali madini huku akisisitiza kuwa, kiu yake binafsi ni kuona taswira
nzuri inajengeka kuhusu sekta hiyo ikiwemo kufanya kazi kwa weledi na kuongeza
kuwa, matokeo bado hayaonekani.
Vilevile,
amewataka watendaji kuchukua hatua badala ya kutumia muda mrefu kutafuta
miongozo wakati wanapotekeleza majukumu jambo ambalo linachelewesha utekelezaji
wa majukumu. “ Unasubiri mwongozo gani ilhali unayo Sheria ya Madini?amehoji
Waziri Biteko.
Pia, amechukua
fursa hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki na kueleza
kuwa, ni kiongozi ambaye amemfundisha mambo mengi.
“Namshukuru
sana dada yangu, rafiki yangu Angellah. Alinipokea vizuri sana. Hakuna
ushirikiano nilioukosa kwake. Amenifundisha mengi ikiwemo kukaa kwenye kikao na
kujadili mambo kwa kina,” amesema Biteko.
Pamoja na
hayo, Biteko ametumia fursa hiyo kumshukuru Naibu Waziri Nyongo kwa kuwa naye
pamoja katika kipindi chote ambacho alikuwa Naibu Waziri katika wizara ya
madini.
Katika hatua
nyingine, Waziri Biteko ameitaka STAMICO kuhakikisha kuwa, inaanza kutoa gawio
kwa Serikali na ikiwezana, jambo hilo lifanyike kabla ya mwaka ujao wa fedha.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, awali akizungumza katika kikao
hicho, amewataka watumishi ambao hawakupata fursa ya kusikia maagizo ya Rais
Magufuli kufanya hivyo ili kila mmoja asimame kwa lengo moja.
“Hatukusemwa
vizuri. Nchi nzima imesikia na dunia imesikia. Tukiendelea hivi,
hatutavumiliwa,” amesisitiza Nyongo.
Pia, ameitaka Tume
ya Madini kuhakikisha inazingatia na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais
Magufuli ikiwemo kutekeleza wajibu wao.
Awali,
akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon
Msanjila amesema kwamba, kikao hicho ni cha kwanza na Waziri Mpya ikiwemo
Mjumbe wa Bodi ya STAMICO na kuongeza kuwa, kinalenga kutoa utambulisho rasmi
wa Waziri Mpya wa Madini na kusikia maelekezo ya Waziri Biteko kufuatia maagizo
yaliyotolewa na Waziri.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo
akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
|
Baadhi ya Watendaji wa Wizara na Taasisi
wakifuatilia kikao hicho
|
Baadhi ya Watendaji wa Wizara na Taasisi
wakifuatilia kikao hicho
|
No comments:
Post a Comment