Na
Asteria Muhozya, Iringa
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wanaomiliki migodi kwa kuvamia
maeneo bila kuwa na leseni, wasimame mara moja.
Naibu Waziri Nyongo
ametoa kauli hiyo katika mgodi wa Ulata
kijiji cha Ulata wilayani Iringa , wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua shughuli za uchimbaji madini ikiwemo
kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wadogo.
Aidha, kauli ya Naibu
Waziri inafuatia mgogoro uliopo katika mgodi huo kati ya mwenye leseni ya kumiliki mgodi huo Ibrahim
Msigwa , wachimbaji wadogo wanaochimba katika eneo hilo na Mansoor Almasi anayetajwa kuwa mmiliki mwingine
na mnunuzi wa madini ya dhahabu
yanayochimbwa mgodini hapo ambaye kwa mujibu wa taratibu, hana vibali vinavyomruhusu kufanya shughuli hizo.
Akilenga kutatua na
kuumaliza mgogoro uliopo mgodini hapo, Naibu Waziri amemtaka Mansoor Almas,
kufika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa ifikapo Januari 15, na endapo
atakiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Sisi kama serikali
ambao ndiyo tunatoa vibali tunamtambua bwana Msigwa kuwa ndiye mmiliki halali.
Nataka kuonana na huyu Mansour na yoyote anayedharau serikali tutakula nae
sahani moja,” alisisitiza Naibu Waziri.
Naibu Waziri alisema
lengo la kutaka Mansour kufika wilayani hapo ni kutaka kusikia kutoka pande
zote ili mgogoro huo uweze kutatuliwa na
kufika mwisho jambo ambalo litawezesha
shughuli za uchimbaji katika eneo husika kuendelea vizuri ili pande zote yaani serikali na wachimbaji
wanufaike.
Akifafanua kuhusu
suala la shughuli za uchimbaji, Naibu Waziri amesisitiza kuwa, ili kuwa
mchimbaji halali ni lazima kuwa na kibali kutoka serikalini na kuongeza kwamba,
ni vigumu kuomba kwenye leseni ya mtu mwingine.
Pia, amewataka
wachimbaji wadogo kutoshirikiana na wale wote wanaopindisha utekelezaji wa sheria na taratibu katika
shughuli za uchimbaji madini na badala yake washirikiane na wale wenye vibali
vya umiliki kutoka serikalini.
Pia, Naibu Waziri
Nyongo aliwataka wale wote wasiokuwa na uwezo wa kuchimba kuingia mikataba na
wachimbaji wengine wenye uwezo ili kuwezesha lengo la kumiliki leseni kutimia
kwa kuhakikisha kwamba zinafanyiwa kazi. “ unaweza kuingia mkataba na
mchimbaji wengine wakiwemo wa kati.
“Nataka muelewe
kwamba, mnaochimba mnachimba kwa niaba ya watanzania kwa sababu watanzania
ambao siyo wachimbaji. Hawa wanafaidika kutokana na kodi na mrabaha unaolipwa
kutokana na shughuli zenu, kwa kuwa fedha hizo zinatumika katika kutoa huduma
nyingine,” alisema Nyongo.
Awali, wachimbaji hao
waliwasilisha kero kwa Naibu Waziri kuhusu mgogoro wa umiliki wa mgodi huo
umesababisha shughuli za uchimbaji mgodini hapo kuwa mgumu suala ambalo
linasababisha ugumu wa kupata kipato cha kujikimu na kuendesha familia zao.
Akitoa utetezi wake
kwa Naibu Waziri kuhusu kero zilizowasilishwa dhidi yake na wachimbaji hao, Msigwa
amesema mazingira mabaya mgodini hapo yaliyowasilishwa na wachimbaji yanatokana
na kuwepo kwa kesi mahakamani jambo ambalo linamfanya ashindwe kuendelea na
shughuli za uchimbaji kama inavyompasa.
Wakati huo, huo, katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Iringa,
Katibu Tawala wa Mkoa huo Happines Seneda, alimweleza Naibu Waziri kuhusu
umuhimu wa kuwa na Afisa Madini wa Mkoa huo badala ya kutegemea AFisa Madini wa
Mkoa wa Njombe jambo ambalo ameeleza kwamba, uwepo wake mkoani humo utaongeza
ufanisi katika ufuatiliaji wa shughuli za madini.
Akijibu ombi hilo,
Naibu Waziri Stanslaus Nyongo alimweleza Katibu Tawala huyo kuwa, Wizara imelenga
kuhakikisha kwamba kila Mkoa unakuwa na Afisa Madini baada ya kuondolewa kwa
Makamishna wa Madini wa Kanda kufuatia Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017.
Naibu Waziri Nyongo
alitembelea mgodi huo Januari 14, 2019.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa
wa Iringa mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kukagua shughuli
za uchimbaji madini. Katikati ni Mkuu wa
Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao chake na watendaji
wa Mkoa wa Iringa kabla ya kuanza ziara ya kukagua shughuli wa wachimbaji
wadogo katika mgodi wa Ulata.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiteta jambo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Hashim
Komba wakati akiondoka katika eneo la
mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata Wilaya ya Iringa, mara baada ya kuzungumza na
wachimbaji wadogo na kutatua mgogoro uliokuwepo mgodini hapo.
![]() |
Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo akikagua mazingira ya shughuli za wachimbaji wadogo
katika mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayai Iringa. Naibu Waziri alifika
mgodini hapo kwa ajili ya kutatua mgogoro baina ya mwekezaji na wachimbaji
ikimweo pia kuzungumz na wachimbaji katika
mgodi huo.
![]() |
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo akiteta jambo na Maafisa alioongozana nao katika ziara ya kukagua na kutatua mgogoro
katika mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayani Iringa.
![]() |
Afisa
Madini Mkoa wa Iringa na Njombe Mhandisi Wilfred Machumu akizungumza jambo
wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri na wachimbaji katika mgodi wa Ulata,
kijiji cha Ulata. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na katikati
ni Katibu Tawala Wilaya ya Iringa, Hashim Komba.
![]() |
Sehemu
ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Mlata, Kijiji cha Mrata, Kata ya Uwasa
Wilaya ya Iringa wakifuatilia mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo. (hayupo pichani).
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali
wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa.
No comments:
Post a Comment