Na
Nuru Mwasampeta
Naibu Waziri wa
Madini Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuwa wazalendo na
waaminifu kwa nchi kwa kulipa kodi stahiki zinazotokana na biashara ya madini
wanayoifanya.
Biteko amesema
anashangazwa kuona kuwa mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa ni
mdogo ilihali asilimia 96 ya shughuli za uchimbaji zinafanywa na wachimbaji
wadogo na asilimia nne tu zimeshikwa na wachimbaji wakubwa na ndio wanachangia
Zaidi katika ukuaji wa pato la taifa.
Biteko amebainisha
kuwa hayo ni matokeo ya ukwepaji wa baadhi ya wachimbaji wadogo katika kulipa
kodi stahiki zitokanazo na uchimbaji wa madini.
Ameyasema hayo leo
tarehe 2 Januari, 2019 wakati akifungua rasmi mafunzo kwa wachimbaji wadogo katika
eneo la Katente mkoani Geita.
Akifungua mafunzo
hayo, Biteko amesema, mnamo mwaka 2016 Serikali ilitenga kiasi cha dola za
kimarekani 3,703,630 kwa ajili ya utafiti wa kina wa jiosayansi chini ya mradi
wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ili kuboresha maisha ya
mchimbaji mdogo na kutatua changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na
uzalishaji mdogo na uchimbaji usiozingatia usalama na afya kwa mchimbaji.
Biteko alibainisha
kuwa kazi ya utafiti katika mji wa Katente umekamilika kama inavyoshuhudiwa
kupitia mafunzo yanayotolewa kwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo yatakayosaidia
kupunguza upotevu wa muda, uharibifu wa mazingira, upotevu wa mitaji pamoja na
upotevu wa madini ya dhahabu yanayotokana na uelewa wa namna ya kufanya kazi
hiyo.
Aidha, Biteko
alibainisha kuwa, Baada ya matokeo ya utafiti huo uliofanywa kwa ushirika baina
ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na
kubaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo katika kukua kiuchumi.
Kutokana na
changamoto zilizobainishwa na utafiti huo, Serikali kupitia Wizara ya Madini
imeanza kujenga madarasa na kufunga mitambo kwa ajili ya mafunzo Zaidi na
kubainisha kuwa eneo la Katente ni moja kati ya maeneo ambayo mafunzo hayo
yatatolewa.
Pamoja na kupewa
mafunzo hayo, Biteko amewataka wachimbaji hao kuunda vikundi na kufanya
shughuli zao ndani ya vikundi ili kuirahisishia Serikali kuwatambua na kuwapa
huduma stahiki zitakazowawezesha kuboresha kazi zao pamoja na afya zao.
Akizungumzia jitihada
zinazofanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo; Biteko
alisema ni pamoja na kuendelea kutenga maeneo maalaum kwa ajili ya wachimbaji
wadogo, kutoa ruzuku, kurahisisha utoaji wa leseni, pamoja na kutoa mafunzo ya
mara kwa mara ili kuwapa wachimbaji wadogo uelewa katika shughuli ya uchimbaji.
Utafiti huo
ulifanyika kufuatia nia na adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais Dr.
John Pombe Magufuli katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanaondokana na
uchimbaji usio na tija na kwenda kwenye uchimbaji utakaoongeza kiasi cha
uzalishaji na baadaye kuongeza kipato kwa wachimbaji wadogo na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Jioloji kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini Tanzania (GST) Maruvuko Msechu alisema mafunzo yanayofunguliwa ni
matokeo ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye lengo la kuhakikisha
watanzania wanafaidika na uwepo wa madini nchini ili kujiondoa katika lundo la
umaskini kwa kuongeza kipato na kuimarisha sekta mtambuka za uchumi.
Msechu alisema,
Utafiti huo ulifanyika katika maeneo ya Ngazo, Kereza, na Katente wilayani
Bukombe ukihusisha matumizi ya taaluma ya jiolojia, jiofizikia, na jiokemia
ukihusisha uchukuaji wa sampuli mbalimbali za udongo na miamba.
Msechu aliongeza kwa
kusema kuwa matokeo ya utafiti huo yalipelekea kufanyika kwa utafiti wa kina
katika eneo la Katente, utafiti ulioanza rasmi tarehe 28 mwezi Oktoba, 2016
ambao ulipelekea jumla ya chorongo 19 za DD na 24 za RC kuchorongwa na
kukusanya jumla ya sampuli 2821.
Aidha aliushukuru
uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Mkuu wa Wilaya pamoja na kamati ya
ulinzi ya wilaya ya Bukombe kwa ushirikiano waliouonesha kipindi chote cha
kufanya utafiti huo.
![]() |
Wachimbaji
wadogo wa madini katika mji wa Katente wakifuatilia kwa makini mafunzo juu ya
uchimbaji wa madini yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Madini
|
No comments:
Post a Comment