Na Mohamed Saif, Katavi
Vyama vya
Wachimbaji Wadogo wa Madini vya Mikoa yote Nchini (REMAs) vimetakiwa
kuwaelimisha Wachimbaji Wadogo umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo yao na
Taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa agizo hilo Februari 24, 2018
kwenye mkutano na Wachimbaji wa madini kwenye machimbo ya Dhahabu ya Wachimbaji
Wadogo ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani
Katavi.
Naibu waziri Biteko alikutana na wachimbaji wadogo kwenye machimbo hayo
ambao walimueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ukosefu wa
vifaa, elimu na maeneo ya uchimbaji.
Biteko aliwahakikishia wachimbaji madini kote nchini kuwa Serikali haina
kikwazo nao na dhamira yake ni kuona wanakua na kufikia uchimbaji wa Kati ama
hata Mkubwa.
“Rais John Magufuli anawajali sana wachimbaji wadogo, anataka kuona
mnakua ili mpate manufaa zaidi kutokana na shughuli zenu hizi lakini pia jamii
inayowazunguka na Taifa kwa ujumla linufaike kupitia nyinyi,”
Hata hivyo Biteko aliwataka wahakikishe wanatimiza wajibu wao wa kulipa
kodi ambayo alisema ikilipwa kwa usahihi manufaa yake ni makubwa kwao wao kama
wachimbaji lakini pia kwa jamii inayozunguka maeneo ya uchimbaji na Taifa kwa
ujumla.
“REMAs waelimisheni wachimbaji kulipa kodi. Hatuwezi kuiendeleza
Tanzania yetu kama mnakwepa kulipa kodi,” alisema Naibu Waziri Biteko.
“Mtakavyolipa kodi, fedha hiyo itatumika kuwaletea na kuwaboreshea
huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na miundombinu mbalimbali,” alisema
Biteko.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuwarasimisha Wachimbaji wa
Madini kwa kuwapatia Leseni za Uchimbaji ili wachimbe kwa kufuata utaratibu
unaotakiwa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na
Marekebisho yake ya Mwaka 2017.
Alisema Sheria husika vilevile inazungumzia suala la uundaji wa Tume ya
Madini yenye jukumu la kusimamia shughuli zote za madini ikiwemo utoaji wa
leseni ambayo alisema itaanza kazi hivi karibuni.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inao wajibu wa kuwaelimisha wachimbaji
wadogo umuhimu wa kulipa kodi ili kuwa na uchimbaji wenye tija na aliagiza
Halmashauri za Wilaya, Ofisi ya Madini na Vyama vya Wachimbaji Wadogo kote
nchini kushirikiana kuelimisha wananchi wajibu wao wa kulipa kodi na umuhimu
wake.
Biteko vilevile aliwahakikishia Wachimbaji hao kupatiwa maeneo ya
kuchimba ambapo alibainisha kuwa leseni za maeneo yasiyoendelezwa zitafutwa na
maeneo hayo kupewa wale wenye nia ya dhati ya kuyafanyia kazi.
![]() Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na Wachimbaji kwenye machimbo ya dhahabu ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi. |
![]() Muonekano wa machimbo ya dhahabu ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi yaliyotembelewa na Naibu Waziri, Doto Biteko. |
![]() Baadhi ya Wachimbaji Wadogo kwenye machimbo ya dhahabu ya Kapanda, Mkoani Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani). |
![]() Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) akisalimiana na Wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya Dhahabu ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi. |
No comments:
Post a Comment