Na
Veronica Simba, Kagera
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amemwagiza mmiliki wa Kampuni inayochakata Madini Bati
ya African Top Minerals iliyopo Kyerwa mkoani Kagera, Hassan Ibar, kutoendelea
na kazi hiyo hadi pale atakapofuata taratibu za kuomba na kupatiwa leseni
halali ya Serikali.
Alitoa agizo hilo
jana Februari 28, alipotembelea na kukagua Kampuni hiyo akiwa katika ziara yake
ya kazi mkoani Kagera.
Naibu Waziri
alimwambia mmiliki huyo kuwa, Serikali inapenda wawekezaji wawepo ili pamoja na
mambo mengine wasaidie upatikanaji wa ajira kwa wananchi lakini akaonya kwamba
kamwe haitaridhia mtu yeyote kufanya uwekezaji pasipo kuwa na leseni halali
itakayowezesha kutambuliwa na Serikali na kulipa kodi zote stahiki.
“Naomba utambue kuwa
unafanya shughuli hii kinyume cha sheria. Hivyo naagiza, kuanzia sasa
usiendelee na kazi hadi pale utakapokuwa na leseni.”
Aidha, Naibu Waziri
pia alitembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kyerwa kuliko na shughuli za
uchimbaji madini ya Bati pamoja na Viwanda kadhaa vya uchakataji Madini hayo,
vikiwemo vya TanzaPlus Minerals na Hamad Mine Scale.
Akizungumza na
wana-kikundi wa Umoja wa Wachimbaji Kyerwa, Naibu Waziri aliwasihi wawe
wavumilivu wakati Serikali ikishughulikia suala la kujisajili na Mikataba ya
Kimataifa itakayowezesha kutambulika kwa Madini ya Bati yanayochimbwa nchini
ili yaweze kuuzwa popote Duniani.
“Natambua mnapitia
kipindi kigumu kutokana na zuio tuliloweka la kutouza Madini ghafi nje ya nchi.
Serikali inashughulikia suala hilo kwa uharaka ili kama nchi, nasi tuweze
kuingia katika Mikataba hiyo ya Kimataifa ambayo itatuwezesha kuleta wawekezaji
mbalimbali hapa, waje wanunue madini yetu hapa kwa ushindani, na tuuze kwa bei
nzuri zaidi tofauti na ilivyo sasa.”
Hata hivyo, Naibu
Waziri aliwataka wachimbaji hao kuachana na suala la utoroshaji wa madini na
kuyauza kwa njia za magendo huku akionya kwamba, yeyote atakayekamatwa,
atawajibika kisheria.
Awali, akizungumza na
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Kanali Shaban Lissu, Naibu Waziri alimsisitiza
kuhakikisha Ofisi yake inaimarisha ulinzi katika njia zote za panya, ili
kudhibiti utoroshwaji wa madini.
Kwa upande wao,
wachimbaji wadogo wa Kyerwa, wakiwasilisha maombi yao kwa Serikali, walimwomba
Naibu Waziri kupatiwa leseni katika maeneo mbalimbali.
Akijibu maombi hayo,
Naibu Waziri aliwaahidi kuwa Leseni zitaanza kutolewa na kuhuishwa mara tu Tume
ya Madini itakapoanza kufanya kazi, ambapo alisema anaamini itakuwa ni hivi
karibuni.
Madini ya Bati yaliyo ghafi. |
No comments:
Post a Comment