Na Greyson Mwase,
Mtwara
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amezitaka halmashauri zote nchini kutokutoza kodi
zilizofutwa kwenye madini ya chumvi ili wazalishaji wa madini hayo waweze
kufanya kazi katika mazingira mazuri na kulipa kodi stahiki serikalini.
Naibu Waziri Nyongo
ameyasema hayo leo Desemba 12, 2018 kwenye mkutano wake na wazalishaji wa
madini ya chumvi kutoka katika Chama cha Wazalishaji wa Madini katika Mkoa wa
Mtwara (MTWAREMA) kilichofanyika kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Mtwara mjini Mtwara ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo
yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kusikiliza na kutatua
kero za wachimbaji wa madini.
Alisema kuwa,
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini iliamua kufuta baadhi ya
kodi walizokuwa wanatozwa wazalishaji wa
madini ya chumvi ambazo zilikuwa ni mzigo kwao na kushindwa kufikia malengo
waliyojiwekea.
“Ninaziagiza
halmashauri zote nchini kutoza kodi kwa kuzingatia sheria zilizopo huku
zikihakikisha kodi zilizofutwa kisheria hazitozwi tena.” Alisema Naibu Waziri
Nyongo.
Akielezea mikakati ya
Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kuwasaidia wazalishaji wa madini ya
chumvi katika mkoa wa Mtwara, Naibu Waziri Nyongo alieleza kuwa ni pamoja
na kuangalia namna ya uanzishwaji wa
kiwanda cha chumvi katika mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuongeza ubora na thamani
ya madini ya chumvi.
Katika hatua nyingine
akizungumza na kikundi cha Umoja wa Vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa
madini ya mchanga katika eneo la Ziwani lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara,
mbali na kupongeza kikundi hicho kwa kazi nzuri Naibu Waziri Nyongo aliomba
Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kuendelea kukisaidia kikundi hicho kwa kuwapa
mikopo ya fedha ili waweze kuzalisha zaidi.
Aidha, aliwataka
wakandarasi wanaopewa zabuni za ujenzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na
majengo kununua mchanga na tofali kutoka katika vikundi vya wachimbaji wa
mchanga katika mkoa wa Mtwara ambao wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa
sheria kwa lengo la kuwainua kiuchumi.
Pia aliagiza Ofisi ya
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuwapa ushauri wa kitaalam
wachimbaji wa madini ya mchanga ili kufanya uchimbaji uwe wenye tija na
kuzingatia sheria na kanuni za madini zilizopo.
Wakati huohuo Naibu
Waziri Nyongo alifanya ziara katika shamba la chumvi linalomilikiwa na jeshi la
magereza la Kiwanda Chumvi lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara na kupongeza
jeshi hilo kwa kazi nzuri.
Kutoka kushoto, Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara,
Mhandisi Ephraim Mushi, Msaidizi wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo,
Mhandisi Noel Baraka wakipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Migodi Mwandamizi
kutoka Ofisi ya Madini ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Aidan
Mhando kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo Wilayani Mtwara
mkoani Mtwara.
Afisa Tarafa wa Ziwani,
Fransis Mkuti (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (kulia) kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo Wilayani
Mtwara mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akichimba mchanga pamoja na wachimbaji wa
madini ya mchanga kwenye eneo la uchimbaji wa mchanga la Ziwani lililopo
Wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akikagua madini ya chumvi katika ghala la kuhifadhi
madini hayo kwenye shamba la chumvi linalomilikiwa na Jeshi la Magereza la
Kiwanda Chumvi lililopo wilayani Mtwara mkoani Mtwara.
Mkuu wa Gereza la
Kiwanda Chumvi lililopo katika Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, SP Mohamed
Mkangumbe (katikati) akionesha moja ya mashamba ya chumvi kwenye ziara hiyo.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wazalishaji
wa madini ya chumvi kutoka katika Chama cha Wazalishaji wa Madini katika Mkoa
wa Mtwara (MTWAREMA) mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika katika
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment