Na Greyson Mwase,
Katavi
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ameagiza Kaimu
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Mkuu wa Wilaya
ya Mpanda, Afisa Usalama wa Wilaya, na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kuhakikisha wanakuwepo wakati wa ufungaji na ufunguaji wa lakiri
(seal) kwenye madini ya dhahabu ili
kudhibiti utoroshwaji wa madini kwenye migodi.
Ameyasema hayo leo tarehe 09 Oktoba, 2018 mara baada ya
kumaliza ziara yake katika Mgodi Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la
Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi
ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika
mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli
za uchimbaji wa madini, kusikiliza na
kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake
Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Salehe Mhando,
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Katavi (KATAREMA),
William Mbongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard
Luyoka, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na waandishi wa
habari.
Alisema kuwa, ni kosa
kubwa la kisheria kwa Afisa Madini Mkazi kufunga au kufungua lakiri (seal)
pasipo kushirikisha Mkuu wa Wilaya,
vyombo vya ulinzi na usalama na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusisitiza
kuwa iwapo itagundulika Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria.
Akielezea mikakati ya
Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini Nchini,
Nyongo alisema kuwa ni pamoja na uboreshaji wa Sheria ya Madini iliyolenga
kuondoa mianya ya utoroshwaji wa madini nje ya nchi kwa kuzuia usafirishwaji wa
madini ghafi nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa,
Serikali inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika ujenzi wa
mitambo ya kuchenjulia madini ndani ya nchi
ili kuyaongezea thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi na kuongeza mapato.
Wakati huohuo
akizungumza katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo, Naibu Waziri
Nyongo alimtaka mmiliki wa leseni kuhakikisha anaandaa mikataba na kusaini
pamoja na wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika
eneo hilo.
Alisema kuwa,
Serikali kupitia Wizara yake haipo tayari kushuhudia migogoro kati ya
wawekezaji na wachimbaji wadogo wa madini pasipo suluhu inayotokana na
ukiukwaji wa Sheria za Madini na kanuni zake.
Katika hatua nyingine,
Nyongo alimtaka mwekezaji huyo kutafuta mwekezaji mkubwa kwa ajili ya usimamizi
wa shughuli za uchimbaji madini katika eneo husika iwapo anakosa uwezo wa
kuendeleza kama leseni ya madini inavyomtaka.
Aidha, alimwelekeza Kaimu
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka kuhakikisha
anatafuta maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini, ili waweze kuchimba
katika mazingira mazuri huku wakifuata sheria na kanuni za madini.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha
wanalipa mrahaba na kodi mbalimbali Serikalini ili mapato yaweze kutumika
kwenye uboreshaji wa sekta nyingine kama
vile afya, elimu, maji na miundombinu.
Awali mbali na
pongezi, wakiwasilisha kero mbalimbali wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha
shughuli za uchimbaji madini katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo
katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo walieleza
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji midogo, vifaa duni pamoja
maeneo rasmi kwa ajili ya uchimbaji madini.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi kabla ya kuanza ziara yake katika mkoa huo yenye
lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa
madini tarehe 09 Oktoba, 2018.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akisalimiana na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi
& Kapufi, Mahmood Yass (kushoto)
kabla ya kuanza ziara yake katika mgodi huo uliopo katika eneo la Singililwa
Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akiangalia sampuli ya makinikia ya dhahabu katika Mgodi
wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani
Mpanda mkoani Katavi.
Meneja Mkuu wa Mgodi
wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi, Mahmood Yass (kulia) akimwonesha Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) moja ya mawe yenye madini ya
dhahabu.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akisalimiana na sehemu ya wafanyakazi wa Mgodi wa
Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa lililopo
Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu
wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Mkaguzi wa Migodi
kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Katavi, Paul Veran (kushoto)
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) kwenye eneo yanapohifadhiwa makinikia ya
dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la
Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kulia) akikagua shughuli za uchenjuaji wa
dhahabu zinazofanywa na wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba
yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi.
Sehemu ya wachimbaji
wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika machimbo hayo.
Kutoka kushoto Katibu
wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Noel Baraka na Mkaguzi wa Migodi kutoka Ofisi
ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Katavi, Paul Veran wakifuatilia maelekezo
yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo
pichani)
Mmoja wa wachimbaji
wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi, Fatuma John akiwasilisha kero yake kwa Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)
Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo
katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani
Mpanda mkoani Katavi (hawapo pichani).
No comments:
Post a Comment