Na Greyson Mwase,
Dodoma
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ametoa siku mbili kwa kampuni inayojishughulisha na
uchimbaji wa madini ya vito katika kijiji cha Kwahemu Wilayani Chamwino mkoani
Dodoma ya Ruvu Gemstone Mining Co. Limited inayomilikiwa na Kimon Dimitri
kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa mpango wa utoaji wa huduma
kwa jamii kwa kipindi cha miaka miwili
kabla ya kutoa maamuzi ya serikali.
Naibu Waziri Nyongo
aliyasema hayo jana tarehe 06 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kwahemu kilichopo Wilayani Chamwino
mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji
wa madini, kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji wa madini pamoja na wananchi wanaozunguka migodi.
Katika ziara yake
Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya
Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Chinolwa, Joel Makanyaga, Kaimu Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Joshua Nduche, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na
waandishi wa habari.
Alisema kuwa, haiwezekani
kampuni inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya vito ya Ruvu Gemstone
Mining Co. Limited ikaendesha shughuli zake pasipo kunufaisha wananchi
wanaozunguka migodi yake.
Aliendelea kusema
kuwa, Serikali kamwe haitamvumilia mwekezaji wa aina yoyote atakayeendesha
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini kwa kukiuka Sheria Mpya ya Madini yenye kipengele kinachowataka wawekezaji
kuchangia katika uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
vituo vya afya, miundombinu ya barabara na shule.
“Serikali kupitia
Wizara ya Madini imejipanga katika kuhakikisha watanzania wote wananufaika na
uwepo wa rasilimali za madini kupitia kodi, tozo mbalimbali pamoja na mpango wa
utoaji wa huduma za jamii,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Alisisitiza kuwa, ni
lazima nakala za ripoti zisambazwe kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani na Mbunge
ili kubaini ukweli wa madai ya mwekezaji
kuwa amekuwa akichangia katika huduma za jamii tangu alipoanza kuchimba madini
ya vito mwaka 1986.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo alimtaka mwekezaji kuhakikisha anadumisha mahusiano na jamii
inayozunguka mgodi ili kuepusha migogoro
inayotokea mara kwa mara.
Awali wakiwasilisha
kero kwa Naibu Waziri Nyongo wananchi wa kijiji hicho walimweleza kuwa tangu
kuanzishwa kwa mgodi husika hawajaona manufaa ya aina yoyote zaidi ya kunyanyaswa
kwa kunyang’anywa ardhi, kupigwa na wakati mwingine kufungwa jela.
Akiwasilisha kero kwa
niaba ya wananchi hao, Daudi Kiloka ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kwahemu
alisema kuwa awali walikuwa na shamba kubwa lenye ukubwa wa takribani heka 500 chini ya Umoja wa Bega kwa Bega wa kijiji
hicho lakini baadaye shamba hilo lilikuja kutwaliwa na mwekezaji huyo.
Aliendelea kusema
kuwa, wananchi wamekuwa wakikosa huduma muhimu ikiwa ni pamoja na shule, maji
na vituo vya afya hali inayolazimu
wananchi wengi kutumia muda mwingi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata
huduma.
Mmiliki wa Mgodi wa
Mawe uliopo katika eneo la Itiso
Wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Sisti Mganga kushoto akielezea shughuli
zinazofanywa na mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili
kutoka kushoto mbele)
![]() |
Moja ya mitambo ya
kukata mawe katika Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga katika eneo la
Itiso lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma
No comments:
Post a Comment