Wednesday, March 28, 2018

Naibu Waziri Biteko-Ukuta wa Mirerani utaweka rekodi Afrika


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Ujenzi wa Ukuta kuzunguka Migodi ya  Mirerani ni jambo la Kihistoria na kwamba linatarajiwa kuweka rekodi Barani Afrika.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo tarehe 23 Machi, wakati wa kikao cha Maandalizi ya Uzinduzi wa Ukuta huo unaotarajiwa kuzinduliwa mapema mwezi Aprili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John  Magufuli.

Aliongeza kuwa, ukuta huo ni jambo ambalo watanzania wamelisubiri kwa miaka mingi licha ya kuwepo kwa mapendekezo na sasa hatua zimechukuliwa na kutekelezwa.

Pia alilipongeza Jeshi kwa nidhamu kubwa ambayo limeonesha kwa ujenzi wa ukuta huo  wenye urefu wa kilomita 25.4  na ambao ujenzi wake umechukua kipindi cha miezi 3 tofauti na ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alilipongeza Jeshi kwa kazi ambayo imefanyika na kuwataka Wajumbe wa Kamati kukamilisha utekelezaji wa majukumu yote kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Simanjiro, Wizara ya Madini,  Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO - Manyara) na Wakala wa Barabara ( TANROAD)


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia), akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti mara baada ya kikao cha Maandalizi ya Uzinduzi wa Ukuta wa Mirerani.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Issa Nchasi, (wa pili kulia) wakibadilishana jambo na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wa Ukuta wa Mirerani.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Issa Nchasi akimweleza jambo Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko mara baada ya kikao cha maandalizi.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa  wa Manyara na Wilaya ya Simanjiro wakibalishana jambo.

No comments:

Post a Comment