Friday, November 16, 2018

Kamati ya ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini yafanya kikao cha kazi


Na Greyson Mwase,

Leo tarehe 16 Novemba, 2018 Kamati ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini  (Local Content) imekutana kwenye Ofisi za Tume ya  Madini zilizopo jijini Dodoma lengo likiwa ni kupokea na kujadili taarifa za kampuni zilizowasilisha mipango  ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini kama sehemu ya maombi ya leseni za madini.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki (kulia) akifafanua jambo katika kikao hicho. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya. 

Wajumbe wa Kamati ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (hayupo pichani) katika kikao hicho. 

Sekretarieti ya kikao hicho ikinukuu maelekezo mbalimbali yaliyokuwa yanatolewa na Mwenyekiti wa  Kamati ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki pamoja na wajumbe wengine katika kikao hicho. 

Mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ringo Iringo akichangia jambo kwenye kikao hicho. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akifafanua jambo katika kikao hicho

Thursday, November 15, 2018

GST yaagizwa kuandaa ramani za Madini ngazi za Mikoa, Wilaya


Ø Biteko asema wachimbaji sasa kuchimba kwa uhakika

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania  (GST) imetakiwa kuandaa ramani zinazoonyesha madini mbalimbali katika ngazi ya Mikoa na Wilaya ili kuwapa nafuu watanzania wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko   baada ya kupokea taarifa ya Utafiti wa Jiokemia katika skeli kubwa na skeli ndogo (Geochemical Mapping for High and Low Density) uliofanyika nchi nzima kwa ushirikiano kati ya GST na Taasisi ya Jiolojia ya China.

Naibu Waziri Doto pia, ameitaka taasisi hiyo kuelekeza nguvu katika kuisaidia serikali katika kupata matokeo chanya katika shughuli za madini huku ikiongeza thamani ya kazi kutokana na utafiti huo na kuongeza kuwa, GST inaweza kutumia utafiti huo mkubwa kuandaa ramani za madini katika ngazi za Mikoa na Wilaya.

 Akizungumzia manufaa ya tafiti huo kwa Tanzania, amesema baada ya muda si mrefu watanzania wanaofanya shughuli za uchimbaji watahamia katika uchimbaji wa uhakika na siyo wa kubahatisha kwa kuwa utafiti huo unaonesha mahali sahihi ambapo shughuli hizo zinaweza kufanywa.

Amesema mbali na shughuli za madini, utafiti huo pia unaweza kutumika katika sekta za kilimo, maji na ujenzi wa barabara kwa kuwa unawezesha kutambua aina ya udongo unaofaa kwa shughuli hizo.

Kutokana na umuhimu wa utafiti na kazi iliyofanywa na taasisi hizo mbili, Naibu Waziri Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuitumia taasisi ya GST katika shughuli za kitaalam ikiwemo kupata taarifa za utafiti zinazohusu sekta ya madini na kuongeza kuwa, sekta hiyo inao uwezo mkubwa wa kutekeleza wajibu wake.

Aidha, Naibu Waziri Doto ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya China kutokana na ushirikiano huo iliyoutoa katika kutekeleza utafiti  huo ambao umegarimu kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 4 na Laki Tano.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jilojia ya China, Profesa Sun Xiaoming amesema kuwa taarifa ya utafiti iliyowasilishwa ni ya nchi nzima ya Tanzania na eneo la Mkoa wa Mbeya.

Amesema utafiti huo umetoa matokeo ya jiokemia ya sampuli 71 nchini kote na sampuli 39 katika mkoa wa Mbeya na kuongeza kuwa utafiti huo utasaidia katika utekelezaji maendeleo ya shughuli za madini, kilimo na mazingira nchini.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mathias Abisai amesema kusudio la ujumbe huo ilikuwa ni kuhakiki kazi iliyofanyika na kuwasilisha ripoti. Ameongeza kuwa, ripoti hiyo itasaidia kwenye tafiti nyingine za madini ikiwemo maji na mazingira.

Ameongeza kuwa, mnamo Mwaka 2009 serikali ya China na Tanzania kwa kutumia taasisi zake za Jiolojia zilisaini hati ya makubaliano (MoU) kwa lengo la kuanzisha mradi huo wa miaka mitano ambapo kazi rasmi ya mradi ilianza mwaka 2013 na kukamilishwa mwaka 2018.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Yokobeth Myumbilwa akileza malengo ya utafiti huo amesema kuwa ni kupata taarifa za utafiti wa jiokemia kwa ajili ya kuandaa kanzidata ambayo itaainisha uwepo wa taarifa zinazo ainisha uwepo wa aina mbalimbali za madini ,upangaji miji ,pamoja na taarifa hizo kuweza kutumika katika shughuli mbalimbali katika  sekta za kilimo  na mazingira.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Taasisi ya Jilojia ya China, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini. 

Naibu Waziri Doto Biteko akimkabidhi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia ya China, Profesa Sun Xiaoming Cheti cha kutambua mchango wake na kukamilika kwa utafiti wa Jiokemia uliofanywa nchini. 

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia ya China, Profesa Sun Xiaoming (kulia) akitoa taarifa ya utafiti huo. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu, Mathias Abisai.

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akionesha taarifa ya utafiti wa jiokemia uliofanywa nchi mzima na Taasisi ya Jiolojia ya Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia ya China. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia ya China Profesa Sun Xiaoming na Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mathias Absai.

Tuesday, November 13, 2018

Mafunzo kuhusu mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato (GePG) yatolewa kwa wahasibu wa Madini


Na Rhoda James, Morogoro                                                

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kufuatilia madeni yote ya ada ya mwaka (Annual Rent) na kutoa muda kwa wahusika ili walipe ada hizo na endapo watashindwa kulipa katika muda watakaopewa, wapelekwe Mahakamani.

Naibu Waziri Biteko ameyasema hayo Novemba 12, wakati akifungua mafunzo ya Wahasibu wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaohudhuria mafunzo hayo yanayohusu Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Mapato (Goverment E- Payment Gateway – GePG). Mafunzo hayo yanafanyika  katika chuo cha Mazimbu Campus Solomn Mkoani Morogoro.

“Serikali inadai madeni mengi ya ada za mwaka, mfano kuna mtu moja ana leseni 103 na anaendela kuomba leseni nyingine lakini pia huyo mtu anadaiwa pesa nyingi za ada ya mwaka,” amesema Biteko.

Naibu Waziri Biteko amesisitiza kuwa lengo la mfumo huo ni kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi zote za Serikali.

Pia, Naibu Waziri Biteko ameongeza kuwa, ili kuleta tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, Mfumo wa GePG umeunganishwa na taasisi zinazotoa huduma za fedha kama vile Simu Benking za NMB na CRDB pamoja na Kampuni za Simu ambazo zinatoa huduma kupitia matawi, mawakala na mitandao ya simu lengo likiwa ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kutumia mfumo huo.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Biteko amesema kuwa mafunzo hayo yapo kisheria na yanatokana na kifungu cha 44 cha Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 (The Finance Act, 2017) ambapo Wizara iliunganishwa rasmi kwenye mfumo huo mwezi Septemba, 2017.

Naibu Waziri Madini Biteko ameongeza kuwa, mnamo tarehe 4 Septemba, 2017 Serikali ilitoa Waraka wa Hazina Na. 3 kuhusu kutumia mfumo wa Serikali wa Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Mapato lengo likiwa ni kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuhusu kujengwa kwa mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato yote ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko amewapongeza Wahasibu wote kwa kufanikiwa kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 310 katika mwaka wa fedha 2018/19 na kueleza kuwa, mpaka kufikia tarehe 31 Oktoba, 2018 jumla ya maduhuli yenye thamani ya shilingi bilioni 111 yamekusanywa ambapo ni asilimia 36 ya lengo ambalo wizara iliwekewa  kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume, Prof. Shukrani Manya amesema kuwa, Mafunzo hayo ni muhimu kwa Tume ya Madini na kwamba yataleta fursa mbalimbali kama vile kujifunza na kuboresha utendaji wa wahasibu katika Tume ya Madini.

Mafunzo kama hayo yalifanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo tarehe 28 hadi 31 Agosti, 2017. Kwa mwaka huu,mafunzo haya yameanza leo Novemba 12 na yanatarajia kukamilika tarehe 15 Novemba, 2018.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza jambo wakati akifungua mafunzo kwa Wahasibu kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini kutoka maeneo mbalimbali nchini (hawapo pichani) wanaohudhuria mafunzo ya Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Mapato Serikalini (Goverment E- Payment Gateway – GePG) katika chuo cha Mazimbu Campus Solomn Maalangu mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo hayo.

Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wahasibu (hawapo pichani) kutoka Wizara ya Madini nchini leo tarehe 12 Novemba, 2018

Naibu Waziri wa Madani, Doto Biteko (kushoto) mara baada ya kusaini kitabu cha wangeni katika Ofisi ya Mratibu wa Chuo cha Mazimbu Campus Solomn Maalangu Dkt. Ibrahimu Mjema mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Madani, Doto Biteko (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na Uongozi kutoka Tume ya Madini na Chuo cha Mazimbu Campus Solomn Maalangu.

Wahasimu kutoka Wizara ya Madini nchini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).

Monday, November 12, 2018

Watalaam wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wapokea taarifa ya mradi wa jiokemia kutoka kwa watalaam wa China Geological Survey (CGS)


Na Samwel Mtuwa, GST

Watalaam wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania-GST) tarehe 10 Oktoba 2018 walikutana na watalaam kutoka Taasisi ya Jiolojia ya China (Geological Survey of China-CGS) kwa ajili ya uwasilishaji na upokeaji wa taarifa ya mradi wa Utafiti wa Jiokemia katika skeli kubwa na skeli ndogo yaani (Geochemical Mapping for High and Low Density) uliofanyika kwa ushirikiano baina ya Serikali ya China na Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Yokbeth Myumbilwa alisema kuwa, Utafiti huo umekusanya taarifa mbalimbali katika upande wa low density na high density  ambapo kwa upande wa low density utafiti ulifanyika katika   Mikoa  ya Mbeya na Songwe na high density ulifanyika kwa nchi nzima .

Akizungumzia juu ya faida zitokanazo na mradi huu wa ushirikiano , Myumbilwa alieleza baadhi ya malengo ya mradi kuwa ni kupata taarifa za utafiti wa jiokemia  kwa ajili ya  kuandaa kanzidata ambayo itaainisha uwepo wa taarifa za jiokemia  za nchini zitakazo ainisha uwepo wa aina mbalimbali za madini, upangaji miji ,pamoja na taarifa hizo kuweza kutumika katika shughuli mbali mbali ndani ya sekta ya killimo  na mazingira.

Alisema kuwa, faida nyingine ni upatikanaji wa taarifa ambazo  zitasaidia pia kuanisha aina mbalimbali za udongo kwa njia ya Ramani yaani (Geochemical Atlas Map of Tanzania).

Mnamo mwaka 2009 serikali ya China na Tanzania kwa kutumia taasisi zake za Geological Survey zilisaini hati ya makubaliano (MoU) kwa lengo la kuanzisha mradi huu wa miaka mitano ambapo kazi rasmi ya mradi ilianza mwaka 2013mpaka 2018.

Akizungumza wakati wa kufunga hafla hiyo, Myumbilwa alishukuru kwa  mafanikio makubwa ya mradi  huo , pamoja ushirikiano mzuri uliokuwepo wakati wa utekelezaji wa mradi toka ulipoanza mwaka 2013.

Katika hafla hiyo ya upokeaji wa taarifa GST iliwakilishwa na watalaam 11  na upande wa China  CGS uliwakilishwa na watalaam Sita Sun Xiaoming ambaye ni mkurugenzi wa CGS, Sun Kai , Wang Huichu , TengXuegian , Li Janjian , Liu Xiaoyangi na Gong Kenghui.


Wizara ya Madini, Mkandarasi SUMAJKT wajadili maendeleo ujenzi wa vituo vya umahiri


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki tarehe Novemba 8, aliongoza kikao cha kujadili Maendeleo ya Ujenzi wa Vituo vya Umahiri vinavyojengwa maeneo mbalimbali nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na Menejimenti ya Wizara ambapo Mkandarasi SUMAJKT na Washauri Elekezi kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects zinazosimamia ujezi wa vituo hivyo walieleza kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa za ujenzi wa vituo hivyo.

Vituo vya umahiri vinajengwa maeneo ya mbalimbali nchini kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya wizara.

Vituo hivyo vinalenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti wa madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Vilevile, vinalenga katika kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo wa madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki alisisitiza kuhusu kuzingatiwa kwa ubora wakati wa  ujenzi wa vituo husika na kusisitiza Mkandarasi SUMAJKT kukamilisha ujenzi huo katika muda uliopangwa.

Vituo vya umahiri viko katika hatua mbalimbali za ujenzi na vinajengwa Bariadi, Bukoba, Handeni, Musoma, Songea, Chunya, Mpanda na Chuo Cha Madini Dodoma.

Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 11.9 zinazotokana na mkopo wa Benki ya Dunia.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki(katikati) Naibu Waziri Stanslaus Nyongo (kulia) na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko wakifuatilia kikao  kati ya wizara  na Mkandarasi SUMAJKT anayejega vituo vya umahiri maeneo mbalimbali nchini na Washauri Elekezi Kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects zinazosimamia ujenzi wa vituo hivyo. Kikao hicho kilijadili maendeleo ya ujenzi wa vituo hivyo.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akieleza jambo wakati wa kikao kati ya wizara na na Mkandarasi SUMAJKT anayejega vituo vya umahiri maeneo mbalimbali nchini na Washauri Elekezi Kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects. Anayefuatilia ni Naibu Waziri Stanslaus Nyongo.

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao hicho.

Mkandarasi SUMAJKT anayejega vituo vya umahiri maeneo mbalimbali nchini na Washauri Elekezi Kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects zinazosimamia ujenzi wa vituo hivyo wakifuatilia kikao hicho baina yao na Wizara. 

Ziara ya Waziri wa Madini yaleta tija kwa STAMICO


Na Bibiana Ndumbaro, STAMICO

Ziara ya Waziri wa Madini Angellah Kairuki (Mb) aliyoifanya tarehe 05.11.2018 katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imeleta tija, baada ya Waziri kuchangia shilingi milioni 24 ili kuongezea nguvu ya kutekeleza mradi Kokoto wa Shirika hilo; uliopo eneo la Ubenazomozi, mkoani Pwani.

Kairuki alitoa mchango huo baada ya kuguswa na tatizo la ukosefu wa mitaji ya kutekeleza miradi, kama lilivyobainishwa katika taarifa ya utendaji kazi ya Shirika hilo iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku; kwenye kikao cha pamoja baina ya Waziri, Wafanyakazi na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila.

Fedha hizo zitaiwezesha STAMICO kufikia bajeti yake ya Shilingi milioni 54 zinazohitajika kufanya utafiti wa kijiolojia unaolenga kubaini ubora wa mwamba katika eneo la Chigongwe, ambapo awamu ya kwanza ya mradi wa kokoto wa STAMICO itatekelezwa.

Waziri Kairuki aliwataka Wafanyakazi kukuza ubunifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi, huku akiwataka kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuboresha utendaji kazi wa STAMICO wenye tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Waziri huyo wa Madini Kairuki na Katibu Mkuu wake Prof. Msanjila, waliipongeza STAMICO kwa kuweka Menejimenti mpya katika Kampuni yake tanzu ya STAMIGOLD kwani imesaidia kujiendesha kwa faida, kuimarisha ulipaji madeni na kumudu gharama za uendeshaji mgodi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku alimshukuru Waziri Kairuki kwa ziara hiyo na ushirikiano anaoutoa kwa STAMICO ili kuhakikisha Shirika linakua kwa kasi na kuleta manufaa mapana kwa Taifa na kwa maendeleo ya Watanzania.

Kanali Mhandisi Ghuliku alimhakikikishia Waziri kuwa STAMICO imedhamiria kuleta mabadiliko katika miradi yake kwa kuboresha miundo mbinu ya miradi, mifumo ya uangalizi na ufuatiliaji na kupunguza gharama za uendeshaji migodi ili kuongeza faida na tija kwa Taifa.
Akitoa neno la shukrani, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa STAMICO Meja Luyodrey Masaki amesema kikao hicho cha pamoja na Mhe. Waziri kimekuwa kichocheo cha uwajibikaji kama Shirika na kwa mtu mmoja mmoja na amemuahidi kuwa STAMICO itarekebisha mapungufu yake na kutoa maoni ya maboresho Wizarani, ili kuleta tija kwa Shirika.

Meja Masaki alimshukuru Kairuki kwa mchango wake wa Shilingi milioni 24 ambazo zitasadia kutekeleza mradi wa kokoto wa Ubenazomozi, na hivyo kuwezesha kukidhi mahitaji ya kokoto katika miradi ya  miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, sambamba na majengo ya biashahara, ofisi na makazi.

Mapema mwezi huu Novemba, Waziri huyo wa Madini aliitembelea STAMICO ikiwa ni ziara yake ya pili kwa mwaka 2018; iliyolenga kufuatilia utendaji kazi wa Shirika, changamoto zake, mbinu utatuzi na mwelekeo wa uendeshaji Shirika kwa kasi itakayoleta matokeo chanya nchini.

Tuesday, November 6, 2018

Wachimbaji Wadogo watakiwa kuhakikisha leseni kutokuwa chanzo cha migogoro


Na Rhoda James, Bukombe

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo nchini kuhakikisha kuwa leseni za uchimbaji Madini zinazotolewa na Wizara kupitia Tume ya Madini ikiwemo mikataba ya ubia wanayongia na Kampuni mbalimbali kutokuwa chanzo cha migogoro nchini.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akisuluhisha mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman ambaye aliilalamikia kampuni hiyo kwa kukiuka mkataba waliojiwekea kati yao.

Akizungumza katika kikao hicho cha usuluhishi, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa, wachimbaji wadogo wanapoingia mikataba na kampuni yoyote ile yenye nia ya kuwa na ubia na Mzawa  ni lazima  wazingatie  na kukubaliana juu ya mikataba wanayoingia  kwa kuwa, pindi  taratibu zinapokiukwa zinaichafua nchi.

 “Mikataba hii mnayoingia mjue ya kuwa nyinyi mnakuwa ni taswira ya nchi sasa mkikiuka mnakuwa mnaichafua nchi yetu, lazima mzingatie makubaliano mnayojiwekea nyie wote, mwekezaji na mzawa,” alisema Biteko.

Aidha, aliainisha baadhi ya masuala ambayo yanatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuingia mikataba na wabia  na kueleza kuwa ni pamoja na kuangalia uhai wa leseni zao, kusajili mikataba yao kwenye Tume ya Madini, kuhakikisha kuwa eneo au biashara wanayoingia haina migogoro, wazawa kujua kuwa wanatakiwa kuwa na asilimia angalau zisizopungua 25 na kuhakikisha kuwa kodi zote za serikali zinalipwa kwa wakati.

Vilevile, Naibu Waziri Biteko alimtaka, Othman ambaye ni mlalamikaji kuhusu ukiukwaji wa mkataba kati yake na Kampuni ya Pamoja Mining Ltd kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria zote ili pande zote mbili ziweze kufanya kazi  kwa tija na bila kukwepa kodi za serikali.

Pia, alitumia fursa hiyo kuzitaka Ofisi za Madini kote nchini kuhakikisha kuwa zinaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili matatizo kama hayo yanayojitokeza sasa yasiendele kujitokeza kwani ni wajibu wa Wizara kuhakikisha kuwa migogoro baina ya wachimbaji  na wawekezaji inakwisha.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda alimshukuru Naibu Waziri Biteko kwa kusuluhisha mgogoro huo ambao umedumu kwa kipindi kirefu nakueleza kuwa, ofisi hiyo itaendelea kuzingatia na kutekeleza maagizo hayo kwa mujibu wa sheria.  


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman (hawapo pichani) katika Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia mbele) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum katika Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Madini Geita na  kampuni ya Pamoja Mining Ltd. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia mbele) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum katika Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Madini Geita na  kampuni ya Pamoja Mining Ltd.