Monday, July 23, 2018

Wanunuzi vito wasiokuwa na mashine za kukata kunyang’anywa leseni


Na Greyson Mwase, Tunduru

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo tarehe 19 Julai, 2018 amesema kuwa wanunuzi wa madini aina ya vito kote nchini wasiokuwa na mashine kwa ajili ya kukata na kung’arisha madini hayo watanyang’anywa leseni kwa kuwa wanaendesha biashara kinyume na taratibu kama Sheria ya Mpya ya Madini ya Mwaka 2017 inavyofafanua.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo katika mkutano wake na wanunuzi wa madini  aina ya vito kutoka Wilaya ya Tunduru uliofanyika mjini Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni kama moja ya sehemu ya ziara yake katika mikoa ya kusini yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo, kuzungumza nao pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.

Alisema kuwa ni kosa la kisheria kwa mnunuzi yoyote wa madini aina ya vito kuendesha biashara pasipo kuwa na mashine za kukatia na kung’arisha  vito.

“Sheria inamtaka mnunuzi ambaye ni mtanzania kuwa na mashine 5 na mnunuzi wa kigeni kuwa na mashine 30 za kukata na kung’arisha madini ya vito, tunataka madini haya yaongeze thamani  ndani ya nchi ili kuongeza mapato serikalini,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko alimtaka Afisa Madini wa Tunduru Mjiolojia Abraham Nkya kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Zuberi Homera na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya kufanya ukaguzi kwenye maduka ya wanunuzi watakaopewa leseni mpya ili kubaini kama wana mashine za kukata na kung’arisha vito na kuchukua hatua za kisheria kwa wanunuzi watakaobainika kutokuwa na mashine hizo ikiwa ni pamoja na kuwaandikia hati za makosa na kuwanyang’anya leseni.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wanunuzi wa kigeni wanaofanya biashara kwa ubia na watanzania kuhakikisha wanawashirikisha kwa kila jambo kama mikataba yao inavyotaka.

Aliendelea kusema kuwa Sheria ya Madini  inamtaka mzawa kuwa na umiliki wa  isiyopungua asilimia 25 kwa kuwa hana uwezo wa kifedha na teknolojia na raia wa kigeni kuwa na asilimia 75 na kusisitiza kuwa ni vyema wakashirikiana kwa kila hatua kwenye biashara ya madini.

“Haiwezekani mbia wa Tanzania hatembelei kabisa eneo la biashara hali inayopelekea kutofahamu  kabisa mwenendo wa biashara na kumwacha mbia ambaye ni raia wa kigeni akifanya kila kitu, hii inapelekea hata madini kutoroshwa nje ya nchi,” alisisitiza Biteko.

Aidha, aliwataka wanunuzi wa madini kuweka kumbukumbu za mauzo za kila siku ili kuweza kufanya ulinganisho wake na madini yanayosafirishwa nje ya nchi ili kujiridhisha  na uwiano wake.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Biteko mbali na kutembelea baadhi ya migodi iliyopo katika kijiji cha Ngapa Mtoni kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma alikutana na wachimbaji wadogo lengo likiwa ni  kukusanya na kutatua kero mbambalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao wa madini ya vito, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini katika kijiji cha Ngapa Mtoni, Abel Kasibila alieleza changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutumia nyenzo duni katika uchimbaji wa madini ya vito, kutokuwepo kwa watafiti ambao wangerahisisha kwenye  ugunduzi wa madini na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki kwenye usafirishaji wa madini.

Alisema changamoto nyingine kuwa ni pamoja na malipo ya leseni kufanyika kwa fedha za kigeni na uwepo wa leseni kubwa bila ya wahusika kufahamika.

Awali akielezea hali ya uzalishaji wa madini ya vito na ujenzi katika wilaya ya Tunduru kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Zuberi Homera alisema takwimu za usafirishaji wa madini ya vito katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni, 2018 zilionyesha kuwa jumla ya gramu 24,279.416 zenye thamani ya Dola za Marekani 108, 807 zilisafirishwa na kulipiwa mrabaha  wa shilingi milioni 14.6.

Aliongeza kuwa jumla ya gramu 1196.01 zenye thamani ya shilingi milioni 160.9 zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa awali wa shilingi  milioni 9.6 katika Ofisi ya Madini Tunduru.

Aliendelea kufafanua kuwa jumla ya tani 1,882 za madini ya ujenzi (mchanga)  zenye thamani ya shilingi milioni 33.9 zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa shilingi milioni 1,050,000.

Aidha alisema kuwa wilaya ya Tunduru ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 85.1 kati ya shilingi milioni 100 iliyopangiwa kukusanya kwa mwaka 2017/2018 sawa na asilimia 85.16.

Akielezea mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli, Homera alisema kuwa wilaya  yake imepanga kutoa huduma za ugani kwa kutoa ushauri kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu uchimbaji bora, salama na unaozingatia utunzaji wa mazingira na kuishauri Wizara ya Madini  kutoa mafunzo kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa wachimbaji wadogo na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yenye madini ili waweze kuelewa Sheria Mpya ya Madini na kanuni zake.

Aliitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuiomba Tume ya Madini kutenga eneo la Ngapa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini katika wilaya ya Tunduru, kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya machimbo na kuhamasisha wenye uwezo kuanzisha viwanda vya kusanifu madini ya vito.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia madini aina ya vito kwenye mchanga kwenye eneo la uchenjuaji katika Mgodi wa Monica Gem uliopo Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akifafanua jambo kwenye mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji cha Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiangalia uchenjuaji wa madini ya vito unaoendelea katika Mgodi wa Monica Gem uliopo Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma tarehe 19 Julai, 2018.

Friday, July 20, 2018

Biteko akunwa na utendaji kazi wa Mgodi wa Kambas


·        Ataka migodi mingine nchini kuiga mgodi huo

Na Greyson Mwase, Songea

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amepongeza utendaji kazi wa mgodi wa kuzalisha makaa ya mawe wa Kambas uliopo wilayani Songea mkoani Ruvuma na kuitaka migodi mingine nchini kuiga mfano kwenye uchimbaji madini kutoka  kampuni hiyo.

Biteko ameyasema hayo leo  tarehe 17 Julai, 2018 kwenye ziara yake aliyoifanya katika mgodi huo uliopo katika kijiji cha  Maniamba wilayani Songea mkoani Ruvuma, lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo pamoja na kutatua changamoto zilizopo.

Katika msafara wake aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya
ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Maafisa Madini wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.

Mara baada ya kupokea taarifa ya shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mgodi huo, Yahya Yusuph Kambaulaya, Naibu Waziri Biteko aliuopongeza mgodi huo kwa kuweza kuzalisha makaa ya mawe na kuuza ndani ya kipindi kifupi tangu imeanza uchimbaji wake Desemba mwaka 2017.

Aidha, aliutaka mgodi huo kuunganisha leseni zake 14 za madini  ili kuweza kuwa wachimbaji wa kati hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa na kuzidi kuongeza mapato Serikalini.

“Kampuni hii imeanza baada ya Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017 ambayo ni rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ndani ya kipindi kifupi wameanza kuchimba kwa mafanikio makubwa, kutoa ajira kwa wazawa na kushiriki katika shughuli za huduma za jamii ( corporate social responsibility), nazitaka kampuni za madini  zote nchini kuiga mfano wa kampuni hii,” alisema Biteko.

Aliendelea kusema kuwa,  ni matarajio yake kuona mgodi wa Kambas unazidi kukua na kuitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,  Halmashauri ya Songea, na Afisa Madini kuulea mgodi huo   huku wakihakikisha unafuata  sheria na kanuni za madini.

Aidha Biteko alitaka halmashauri kutumia fedha inazopata kama mapato kwenye mgodi huo kwenye uwekezaji mwingine mbadala kama vile shule, vituo vya afya na barabara ili kuacha kumbukumbu nzuri katika vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliutaka mgodi wa Kambas kulipa kodi stahiki serikalini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si hapa mgodini, hivyo ninaona ni vyema niwaambie mapema ili kusijitokeze kasoro baadaye,” alisisitiza Biteko.

Aidha, Biteko aliwataka wananchi walioajiriwa  katika mgodi wa Kambas kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutoa ushirikiano kwa mwekezaji huyo mwenye nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi hao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme mbali na kumpongeza Naibu Waziri Biteko kwa usimamizi makini wa  sekta ya madini nchini aliongeza kuwa, ofisi yake ipo tayari kushirikiana na mwekezaji huyo pamoja na kutatua changamoto zitakazojitokeza.

Awali, akiwasilisha taarifa ya uzalishaji, Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya alisema kuwa uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ambapo mpaka sasa wameshachimba tani 5138.

Alifafanua kuwa tani hizo zilichimbwa kwa muda wa miezi mitatu ya Desemba 2017, Mei, 2018 na Juni, 2018 na kuendelea kufafanua kuwa kati ya kipindi cha Januari hadi Aprili, 2018 shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe zilisimama kutokana na mvua kubwa.

Aliendelea kusema kuwa, kuanzia Julai 2018 uzalishaji wa makaa ya mawe kwa siku ni tani 200 na kusisitiza kuwa malengo ya mgodi ni kuzalisha  tani 600 hadi 700 kwa siku ambapo kwa mwezi mgodi utakuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya tani 18,000 hadi 21,000.

Akielezea manufaa ya mgodi wa Kambas, Kambaulaya alisema mgodi umeweza kulipa serikalini kodi mbalimbali inayotokana na mauzo ya makaa ikiwa ni pamoja na mrabaha na ada ya ukaguzi  shilingi milioni 16,  shilingi milioni 4.1 katika kijiji cha Maniamba kama mchango kwa huduma za jamii.

Alisema pia mgodi wake ulichangia katika huduma za kijamii katika ujenzi wa Shule ya Msingi Mipeta iliyoezuliwa paa na upepo mwezi Desemba, 2017 kwa kutoa vifaa vya viwandani vyenye thamani ya shilingi milioni tano na ukarabati wa ofisi ya kijiji cha Maniamba kupitia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni nne.

Kambaulaya aliendelea kusema kuwa mgodi wa Kambas pia umefanikiwa kutoa ajira 20 rasmi na zisizo rasmi 50 hivyo kukuza uchumi wa wananchi wanaozunguka mgodi.

Akielezea maratajio ya mgodi wa Kambas, Kambaulaya alisema mgodi unatarajia kupanuka zaidi kwa kuanzisha mchakato wa uzalishaji wa umeme unaotokana na makaa ya mawe kwa kushirikiana na kampuni ya BBIC kutoka Chini ambapo mpaka sasa wameshasaini makubaliano ya awali ya namna ya kujenga mtambo  wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wenye uwezo wa Megawati 500 hadi 1000 ambapo  umeme huo utaingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Aidha, akielezea changamoto za mgodi huo Kambaulaya alieleza kuwa ni pamoja na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki katika usafirishaji wa makaa ya mawe na kutafuta njia sahihi ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kulingana na tabaka la makaa yanayopatikana katika eneo hilo.
Mhandisi Uchimbaji wa Mgodi wa Kambas, Himid Didi (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati).
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na watumishi pamoja na watendaji wa Mgodi wa Kambas.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati waliokaa mbele), Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (wa tatu kushoto waliokaa mbele), Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema ( wa tatu kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Mgodi wa Kambas.

Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (wa pili kushoto). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya (katikati) akielezea shughuli za kampuni hiyo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko ( wa pili kushoto mbele) kwenye ziara yake katika mgodi huo uliopo katika kijiji cha Maniamba kilichopo Songea mkoani Ruvuma. Kushoto kabisa mbele  ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati mbele), Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme wakiendelea na ziara katika eneo la Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas uliopo Songea mkoani Ruvuma.
Shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe zikiendelea katika Mgodi wa Kambas.

Thursday, July 19, 2018

Waziri Kairuki akutana na Shirikisho la Madini la nchini India


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry) ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Uongezaji Thamani Madini ya Mawe yenye thamani ya Granite na Mable.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 18 Julai, jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki ameueleza ujumbe huo kuhusu adhma ya Tanzania kukakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa vinu vya kuyeyusha madini ya metali, usonara pamoja na ukataji na ung’arishaji madini ya vito hususan madini ya Tanzanite ambayo kwa kiasi kikubwa yamekua yakisafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi.

“Sheria yetu ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017, imekataza usafirishaji wa Makinikia pamoja na madini ghafi nje, ndiyo maana tunakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini ndani ya nchi,” amesema Waziri Kairuki.

Pia, Waziri Kairuki amewashauri wawekezaji hao kukutana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuona namna bora ya kushirikiana katika miradi mbalimbali ikiwemo ya mawe yenye thamani, bati na madini mengine.

Vilevile, Waziri Kairuki amelitaka shirikisho hilo kuona namna ambavyo linaweza kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini nchini hususan katika masuala ya masoko na mitaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini ya Granite na Sekta ya Mawe la nchini India, Keshava Murthy, amemweleza Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo liko tayari kuwekeza kwenye madini ya granite pamoja na marble kwa kuanza na makontena kati ya 20-50 kwa mwezi.

Pia, Murthy ameongeza kuwa, Shirikisho hilo lina wanachama zaidi ya 1200 ambao wanajihusisha na shughuli za uongezaji thamani madini ya granite nchini humo.

Kuhusu ushirikiano na STAMICO, Murthy amemwahidi Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo litakutana na shirika hilo kwa lengo la kubadilishana ujuzi ikiwemo kuangalia namna bora ya kushirikiana katika sekta husika.

Aidha, amemweleza Waziri Kairuki kuhusu maonesho ya  mawe yenye thamani yanayojulikana kama STONA FARE ambayo huandaliwa na shirikisho hilo  na kuongeza kuwa, ni miongoni mwa maonesho makubwa duniani.

Mbali na kukutana na Waziri Kairuki, wawekezaji hao wanatarajia kuendelea na ziara jijiji Dodoma ambapo wanatarajia kukutana na na Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania, kutembelea Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye uchimbaji wa Granite jijini Dodoma.

Kabla ya kuja nchini, wawekezaji hao walitembelea nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji kwenye madini hayo.

Kikao hicho pia, kimehudhuriwa na Mwakilishi kutoka Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TIC), Wataalam kutoka Wizara ya Madini wakiongozwa na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki Mhandisi Ally Maganga aliyemuwakilisha Kamishna wa Madini.


Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini ya Granite na Viwanda vya Mawe la nchini India, Keshava Murthy, akiweleza jambo Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) akiongoza kikao kati ya Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry).

Wednesday, July 18, 2018

Biteko afanya ziara Mgodi wa Tancoal


·        Aagiza  mgodi kulipa kodi stahiki kwa mujibu Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 badala ya Sheria ya Madini ya Mwaka 1998
·        Alishauri shirika la NDC kupeleka haraka mwakilishi wake kwenye mgodi huo

Na Greyson Mwase, Mbinga

Naibu Waziri wa Madini,  Dotto Biteko leo tarehe 17 Julai, 2018 amefanya ziara katika mgodi wa Makaa ya Mawe wa Tancoal uliopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Katika msafara wake aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya
ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Maafisa Madini wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,  pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Mbinga.

Mara baada ya kufika katika mgodi huo na kupewa taarifa  juu ya shughuli za uendeshaji  wa mgodi huo,  Naibu Waziri Biteko aliagiza mgodi huo kuhakikisha unalipa kodi stahiki ya madini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si hapa mgodini, na ninatoa mwezi mmoja mhakikishe mmerekebisha kasoro zote na fedha ambazo hazikulipwa zilipwe. Ninatamani mimi niwe wa mwisho kuliongelea suala hilo, migodi mingine yote imeshaanza kutekeleza sheria hii sijui kwanini mmebaki ninyi,”alisema Biteko.

Alisema ni wakati sasa kwa wananchi wa Tanzania kunufaika na rasilimali za madini kupitia kodi stahiki ambazo zinatumika katika kukuza sekta nyingine ikiwa ni pamoja na   huduma za kijamii.

Alisisitiza kuwa, endapo hatua husika hazitachukuliwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaandikia mgodi hati ya makosa itakayopelekea kunyang’anywa leseni ya uchimbaji na uuzaji wa madini.

Aliongeza kuwa ni jukumu la kampuni ya Tancoal kusafirisha madini hadi eneo la wanunuzi kwa kuwa wana leseni za uchimbaji na uuzaji na si wanunuzi wasio na leseni hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria za Madini.

Pamoja na kuitaka kampuni ya  Tancoal kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria alishauri kampuni hiyo kufanya kazi kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na mbia wake ambaye ni Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kupitia usimamizi  wa uzalishaji, upimaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Aidha, Naibu Waziri  alisikitishwa na kitendo cha NDC kutokuwa na mwakilishi wake hapo mgodini toka mwaka 2016 baada ya afisa aliyekuwepo kustaafu.

“ Ninajua NDC hampo Wizara ya Madini, lakini mpo Serikalini na mimi ni Naibu Waziri wa Serikali hii ninawashauri mlete haraka mwakilishi kwenye mgodi huu ili kuwepo na jicho la NDC kama mbia kwenye mgodi huu badala ya kutegemea taarifa za mbia wenu tu ambaye ni Tancoal,”alisisitiza.

Wakati huo huo akizungumza katika mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa  mara baada ya taratibu kukamilika leseni za biashara ya madini zinatarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwezi huu na kuwataka kujiandaa na soko litakalotokana na wanunuzi wengi watakaojitokeza.

Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka maafisa madini nchi nzima kusikiliza kero za wachimbaji wadogo wa madini pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

Aliwataka wachimbaji madini kuhakikisha wanafanyia leseni zao kazi na zile ambazo zitaonekana hazifanyiwi kazi kwa muda mrefu zitafutwa na kupewa wachimbaji wadogo.

Aidha alisisitiza wamiliki wa migodi ya madini  nchi nzima kuajiri watanzania wenye uwezo kama  Sheria ya Madini inavyofafanua badala ya kuajiri raia wa kigeni tu.

Aidha, Naibu Waziri Biteko mbali na kumpongeza Rais John Magufuli kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi, aliwataka wachimbaji wa madini kumuunga mkono kupitia uzalendo kwenye usimamizi wa madini kwa manufaa ya Taifa.

“Tunataka madini haya baada ya miaka kadhaa yalete matunda kama vile huduma za jamii hususan elimu, hospitali, barabara nzuri n.k” alisisitiza Biteko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme mbali na kumpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa anayofanya katika usimamizi wa sekta ya madini alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga kupima maeneo  maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara kati ya wachimbaji hao na wakulima au wafugaji.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kulia mbele) na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (katikati) wakiendelea na ziara katika eneo la mgodi wa Tancoal uliopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 17 Julai, 2018.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiangalia moja ya jiwe la makaa ya mawe. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akitoa maelekezo kwa baadhi ya watumishi wa kampuni ya Tancoal.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini (hawapo pichani) katika eneo Masuguru lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini katika eneo Masuguru lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakifuatilia  ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani).

Tuesday, July 17, 2018

Biteko abaini masanduku 209 ya sampuli za madini yaliyotelekezwa


·   Aaagiza sampuli kukabidhiwa GST na wahusika kutafutwa popote.

Na Greyson Mwase, Songea

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo tarehe 16 Julai, 2017 amefanya ziara katika mkoa wa Ruvuma lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo pamoja na kusikiliza kero mbalimbalimbali.

Katika ziara yake aliambatana na  wataalam kutoka  Wizara ya Madini, Maafisa Madini wa Songea, Kulwa Kabadi na Mhandisi George Wandinha, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.

Akiwa katika eneo la Madiba lililopo wilayani Songea mkoani Ruvuma, Naibu Waziri Biteko alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa mwananchi mmoja, Allan Mbilinyi kunakoelezwa kuhifadhiwa masanduku 209 ya sampuli za madini ya aina mbalimbali  na kushuhudia masanduku hayo yakiwa yametelekezwa bila kuwa na dalili za aina yoyote ya usafirishwaji.

Awali Naibu Waziri Biteko alipewa taarifa na wananchi ambao ni wasamaria wema kutoka katika eneo la Madaba juu ya uwepo wa sampuli za madini hayo na kusisitiza kuwa  hatua hiyo inatokana na kuunga mkono kasi ya Serikali ya Awamu ya  Tano kupitia  Wizara ya Madini kwenye ulindaji  wa  rasilimali za madini.

Walisema kuwa, tofauti na sampuli za masanduku 209 ya madini ya aina mbalimbali yaliyotelekezwa, kipindi cha nyuma walishuhudia mzigo mkubwa wa masanduku yenye sampuli za madini ya aina mbalimbali yakisafirishwa kutokea eneo yalipotelekezwa masanduku husika.

Naye Naibu Waziri Biteko aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa za madini yaliyotelekezwa alielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia na kumpatia taarifa kabla ya kufika na kuthibitisha na kusisitiza kuwa aliamua kufika ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua za kisheria.

Hata hiyo baada ya kufika eneo husika, Waziri Biteko aliangalia mkataba uliosainiwa kati ya kampuni ya Sino Hydro kutoka China na Allan Mbilinyi kuhusu uhifadhi wa madini hayo na kubaini kutokuwepo kwa kibali cha serikali jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

“Ni kosa la kisheria kuhifadhi madini ya aina yoyote ndani ya mahali popote bila ya Serikali kuwa na taarifa, faini yake ni kubwa pamoja na kifungo,” alisema Biteko

Biteko alielekeza sampuli za madini kuwa chini ya uangalizi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema kabla ya kukabidhiwa kwa Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini thamani halisi. 

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini katika ufuatiliaji wa madini na kusisitiza kuwa Serikali itahakikisha wahusika wanakamatwa sehemu yoyote na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma, Biteko mbali na kuwapongeza wananchi kwa uzalendo wa kutoa taarifa kuhusiana na uhalifu unaofanywa na watu wasio waaminifu kwenye sekta ya madini, aliwataka wananchi hao kuendelea kulinda rasilimali za madini na kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha Naibu Waziri Biteko akizungumza kwa nyakati tofauti katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme alisema kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la  Taifa ikiwa ni pamoja na maboresho ya Sheria ya Madini inayomtambua mtanzania kama mmiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini nje ya nchi.

Aliwataka wachimbaji madini wanapopata leseni kujitambulisha kwanza kwa viongozi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na kijiji pamoja na kulipa fidia kwa wananchi  kabla ya kuanza shughuli zozote za madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema kuwa atafuatilia kila hatua ya namna taarifa zilivyofikishwa Serikalini kuhusu madini yaliyotelekezwa na hatua zilizochukuliwa pamoja na wahusika wote kabla ya  hatua za kisheria kuchukuliwa.

Wakati huohuo Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa ya usimamizi  wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu shughuli za madini kwa kila mkoa na kuchukua  hatua stahiki pale inapohitajika.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akimsikiliza Allan Mbilinyi (wa pili kushoto) ambaye masanduku 209 yenye sampuli za madini mbalimbali yalitelekezwa na kampuni ya Sino Hydro kutoka China, nyumbani na kwake katika kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Sehemu ya masanduku 209 yenye sampuli za madini mbalimbali yaliyotelekezwa  na kampuni ya Sino Hydro kutoka China, nyumbani kwa Allan Mbilinyi katika kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia sehemu ya sampuli za madini yaliyotelekezwa.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na wananchi wa Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.



Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (kulia) kabla ya kuanza ziara yake katika mkoa huo.

Monday, July 16, 2018

GST inazo fursa nyingi za kibiashara-Prof. Msanjila


Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inazo fursa nyingi ambazo zingeweza kuifanya kuwa Taasisi inayoingiza mapato makubwa.

Prof. Msanjila ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo iliyolenga kujifunza namna GST inavyotekeleza majukumu yake, kufahamiana na watumishi wa taasisi hiyo na kufahamu changamoto zinazoikabili.

Kutokana na fursa za kibiashara zilizopo katika taasisi hiyo, Prof. Msanjila ameishauri kujikita katika kutoa huduma za kibiashara kutokana na uwezo iliyonayo na huduma inayotoa kwa jamii hususan wadau wa Sekta ya Madini nchini.

Amesema umuhimu wa GST bado haujatumika katika namna inavyotakiwa na kueleza kuwa, kutokana na Mabadiliko yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, yamelenga kuipa uzito taasisi hiyo.

Pia, Prof. Msanjila amewataka watumishi wa GST kuwa na udhubutu na kila mmoja kuwajibika kikamilifu katika eneo lake analofanyia kazi na pindi wanapohitaji mwongozo kutoka wizarani, wasisite kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine, Prof. Msanjila ameipongeza taasisi hiyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza kuwa, Wizara ya Madini imepata sifa kubwa kutokana na namna GST ilivyotekeleza majukumu yake kikamilifu.

“Taasisi yenu imechangia sana kwenye sifa ilizopata wizara wakati wa uwasilishaji wa Bajeti yake mwezi Mei, nawapongeza sana kwa utendaji kazi, matokeo yenu tunayaona,” amesisitiza Prof. Msanjila.

Vilevile, ameishukuru kutokana na namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wizara na kusema kuwa, “ kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya wizara na taasisi. Mimi, Waziri na Naibu Mawaziri tunashukuru,”

Akizungumzia suala la kuwaendeleza watumishi, amesema kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha kwamba watumishi wanajiendeleza kielimu na kuongeza kuwa, tayari imeanza mchakato ili watumishi waweze kupata nafasi za ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali.

“Tunakamilisha suala la kupata ufadhili. Wenye nia ya kusoma nafasi zitakuwepo. Binafsi napenda sana watu waende shule na hasa vijana,” amesema Prof. Msanjila.

Katika ziara hiyo, Prof. Msanjila ametembelea Idara mbalimbali za GST ikiwemo maabara mbalimbali za utambuzi wa madini na utengenezaji wa ramani mbalimbali za madini.

Awali, Prof. Msanjila alifanya kikao na Menejimenti ya GST, pamoja na kuzungumza na watuishi wa taasisi hiyo. Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu ameambatana na Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu, Issa Nchasi.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiangalia sampuli za madini kupitia darubini ndani ya Maabara ya Utafiti wa Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST). Katibu Mkuu amefanya ziara GST ya kuangalia kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) baada ya kutembelea kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akipewa maelezo juu ya vifaa mbalimbali vya utafiti wa miamba na madini kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiolojia wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Maruvuko Msechu.

Friday, July 13, 2018

Biteko akamata tani saba za madini ya vito yaliyofichwa ndani


Na Greyson Mwase, Morogoro

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amekamata madini  ya vito aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba yaliyokuwa yamefichwa nyumbani kwa mchimbaji wa madini hayo, Juvenal Mnene ambaye ni mmiliki wa kampuni ya J. J. Mnene & Partners na kuamuru kukabidhiwa Serikalini pamoja na mmiliki huyo kufikishwa mahakamani.

Naibu Waziri Biteko amekamata madini hayo katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro lengo likiwa ni kukagua shughuli za wachimbaji wadogo  wa madini ya vito na ujenzi na kutatua changamoto mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Biteko aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Gairo, Madiwani na Mwakilishi wa Mbunge wa Gairo.

Mara baada ya kuwasili katika mgodi wa mchimbaji huyo uliopo eneo la Rubeho, Bitteko alibaini kuwa  mchimbaji huyo alikuwa amelipa mrabaha wa shilingi 400,000 tu tangu mwaka 2013 ndipo akataka kupewa taarifa ya uzalishaji  na kiasi cha malipo yaliyolipwa serikalini ikiwa ni pamoja na kodi mbalimbali ambapo alielezwa na mmiliki wa mgodi huo Juvenal Mnene kuwa  taarifa ya uzalishaji wa madini hayo na vielelezo vya malipo yaliyofanyika serikalini ipo nyumbani.

Naibu Waziri Biteko pamoja na msafara wake alielekea nyumbani kwa mmiliki wa mgodi huo, ambapo alishuhudia madini ya vito aina ya Rhodilite yakiwa yamerundikwa kwenye chumba kimoja na kufungwa kwa kufuli bila kuwekwa lakiri (seal) ya serikali kinyume na sheria ya madini inavyotaka.

“Huu ni utoroshwaji wa madini kwasababu haiwezekani madini yahifadhiwe ndani ya chumba bila serikali kufahamu na kuweka lakiri, na kama serikali hatuwezi kukubali kuona madini yakitoroshwa nje ya nchi na wachimbaji wa madini wasio waaminifu,” alisema Biteko

Katika hatua nyingine, Biteko alibaini mchimbaji huyo alikuwa na mtambo wa kuchenjua madini hayo  nyumbani kwake kwa nyuma bila kuwa na leseni ya uchenjuaji madini kama sheria ya madini inavyotaka.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo, Naibu Waziri Biteko alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Musa Mwakasula kwa kushirikiana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kukamata madini hayo kuyapima ili kujua kiasi chake halisi na kisha kumfikisha mtuhumiwa katika vyombo vya sheria.

Aliongeza kuwa Wizara ya Madini itawachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika na mchakato mzima wa kuficha madini hayo.

“ Haiwezekani kabisa juzi juzi  tumekamata madini yenye uzito wa tani 75 jijini Dar es Salaam, ni lazima tuhakikishe tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote ili ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisisitiza Biteko.

Wakati huo huo, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani Gairo mkoani Morogoro, Naibu Waziri Biteko alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa wa uchumi wa nchi kwa kuboresha sheria za madini.

Alifafanua kuwa, Wizara ya Madini ipo katika mchakato wa kurasimisha  wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni  mara baada ya taratibu kukamilika ili kuondokana na umaskini kutokana na kujiajiri

Alisema kuwa, awali rasilimali za madini zilichukuliwa kama umiliki wa wawekezaji wa nje ya nchi lakini mara baada ya maboresho ya Sheria ya Madini wananchi sasa wana haki zote za umiliki wa rasilimali za madini.

Akizungumzia suala la bei elekezi kwenye madini ya ujenzi, Biteko alisema Serikali ipo katika mpango wa kukaa na wanunuzi wa madini hayo hasa wenye viwanda vya kutengeneza marumaru( tiles) na kukubaliana bei ambayo itafanywa kuwa bei elekezi ya madini hayo ili wananchi wanufaike.

Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka wachimbaji hao kulipa kodi mbalimbali na kufuata kanuni na sheria za uchimbaji madini.

Wakati huo huo akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe alieleza changamoto mbalimbali katika uchimbaji madini katika wilaya yake kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini kutokuwa na leseni kwa kisingizio wameshawasilisha maombi yao kwenye ofisi za madini, kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa uchimbaji madini na kutokuwepo kwa sehemu za kuhifadhia madini.

Aliendelea kusema  changamoto nyingine kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji hususan kwa wachimbaji wadogo wa madini na upatikanaji wa soko la uhakika la madini hayo.


Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe (kushoto) akielezea shughuli za uchimbaji madini katika wilaya yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) kwenye ziara yake katika eneo la Rubeho wilayani Gairo mkoani Morogoro tarehe 11 Julai, 2018.

Mchimbaji madini aliyekamatwa akiwa amehifadhi madini aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba nyumbani kwake, Juvenal Mnene (katikati) akionyesha nyaraka mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko. 

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akimhoji Mchimbaji madini aliyekamatwa akiwa amehifadhi madini aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba nyumbani kwake, Juvenal Mnene (kulia). 

Sehemu ya madini ya vito aina ya Rhodilite yaliyokamatwa nyumbani  kwa mchimbaji Juvenal Mnene katika mtaa wa Magoweko kwenye halmashauri ya mji wa Gairo mkoani Morogoro. 

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani Gairo mkoani Morogoro (hawapo pichani)katika mkutano wa hadhara. 

Sehemu ya na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani Gairo mkoani Morogoro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.